• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
SHINA LA UHAI: HIV mkuki kwa vijana, kunaendaje?

SHINA LA UHAI: HIV mkuki kwa vijana, kunaendaje?

Na PAULINE ONGAJI

KAMA watoto wengine wa kawaida wanaolelewa kijijini kuliko na maisha magumu, ndoto yake Kimutai Kemboi, 28 ilikuwa kujiimarisha na kujikwamua kutokana na umaskini uliokuwa umeikumba familia yake.

Kwa hivyo, alijitihada kufanya vyema shuleni angalau kujihifadhia nafasi chuoni na kusomea mojawapo ya taaluma alizoenzi; udaktari, uhandisi au urubani.

Lakini Novemba 2015, wakati huo akiwa na miaka 24, ndoto yake ilionekana kufikia kikomo alipogundua kwamba alikuwa ameambukizwa virusi vinavyosababisha HIV.

“Katika pitapita zangu jijini, nilipitia karibu na kituo cha VCT ambapo wahudumu walinishawishi nifanyiwe uchunguzi kujua hali yangu ya HIV,” aeleza.

Kulingana na Kemboi, alipigwa na butwaa matokeo yalipoonyesha kwamba alikuwa na virusi, licha ya kuwa alikuwa na uhakika kwamba ni buheri wa afya.

“Sikuamini niliyoyasikia na nikadhani kwamba uchunguzi huo ulikuwa na makosa. Kwa hivyo nilifanyiwa chunguzi zaidi na zote zilithibitisha matokeo ya awali,” asema.

Kwa mwaka mmoja, hakukubali hali yake huku akijaribu kutafakari ni wapi na lini alipoambukizwa virusi hivi? “Mawazo yote yalinielekeza kwa mwajiri wangu wa zamani ambapo baada ya kufanya uchunguzi, niligundua kwamba alikuwa amefariki miezi kadha iliyopita baada ya kuugua maradhi ambayo sikufichuliwa huku nikielezwa kwamba alikuwa amekataa kupokea matibabu,” aeleza.

Je, ni kwa nini mawazo yake yalimwelekeza kwa mwajiri wake?

Kutokana na kuwa familia ya Kemboi ilikuwa maskini, wazazi wake walikabiliwa na changamoto ya kumpeleka shuleni pamoja na nduguze hivyo akalazimika kuacha shule ili kusaka ajira.

“Nilipokuwa katika shule ya upili ilikuwa vigumu kupata karo, na hivyo wakati mwingi nilibaki tu nyumbani wenzangu wakielekea shuleni. Hatimaye nililazimika kuacha shule na kutafuta ajira,” anasema.

Kwa hivyo alisafiri hadi jijini Nairobi kusaka ajira.

“Sikuwa na pesa wala fursa yoyote nilipowasili jijini,” anasema.

Kwa bahati nzuri, alifanikiwa kupata kazi kama mwangalizi wa bustani, ajira iliyokuja na vinono ikiwa ni pamoja na makazi katika ua la nyumba ya mwajiri wake.

Muda si muda uhusiano baina yake na mwajiri wake uligeuka kuwa wa karibu, suala lililomsababisha kupewa chumba cha kulala, ndani ya jumba la bosi.

“Siku moja bosi aliniahidi kunirejesha shuleni iwapo ningemtimizia sharti moja tu. Mwanzoni sikujua alichokuwa akitaka, lakini wiki moja baadaye alinijia na kuniambia nishiriki naye tendo la ndoa bila kinga, ombi ambalo nilitimiza bila wasiwasi,” asema.

Hata hivyo, ile ahadi ya kurejeshwa shuleni iligonga mwamba baada ya mwajiri wake kupoteza ajira na kumfurusha mwishowe huku akidai kwamba hakuwa na pesa za kuendelea kumlipa.

Kemboi anawakilisha idadi inayozidi kuongezeka ya vijana walioambukizwa virusi vya HIV kabla ya kutimu miaka 25.

Uchanganuzi mpya wa utafiti wa mwaka jana wa Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Ukimwi- NACC kudadisi viwango vya maambukizi ya virusi vya HIV, ulionyesha kwamba idadi ya vijana kati ya miaka 15 na 24 wanaoambukizwa maradhi haya imekuwa ikiongezeka.

Kulingana na uchanganuzi huo uliotangazwa majuma machache yaliyopita, kati ya watu watano wazima wanaoambukizwa virusi vya HIV, wawili ni vijana kati ya miaka 15 na 24, ambapo idadi hii inawakilisha asilimia 40 ya maambukizi.

Aidha, vijana katika mabano haya kiumri waliwakilisha asilimia 10 ya vifo vyote vilivyosababishwa na maradhi ya Ukimwi.

Mwaka jana, mkurugenzi wa baraza hili Dkt Nduku Kilonzo alionyesha wasiwasi wake kutokana na idadi iliyokuwa ikiongezeka ya vijana waliokuwa wakiambukizwa virusi vya HIV.

Uchanganuzi huu unaambatana na utafiti wa mwaka wa 2015 ulioongozwa na shirika la muungano wa watu wanaoishi na virusi vya HIV (GNP+) ulioonyesha kwamba vijana katika mabano haya ya kiumri nchini Kenya wanawakilisha zaidi ya nusu (51%) ya maambukizi mapya ya HIV, ongezeko kutoka asilimia 29 mwaka wa 2013.

Kisa na maana?

• Kudorora kwa maadili

Joshua Gitonga, mkuu wa ukaguzi na udadisi katika shirika la NACC anasema kwamba matokeo hayo ni ishara ya kudorora kwa maadili miongoni mwa vijana.

Kulingana naye, vijana wanaanza kujihusisha na masuala ya mapenzi mapema maishani, suala linalowaweka katika hatari ya kuambukizwa maradhi ya zinaa.

Aidha Bw Gitonga anasema kwamba wazazi wanapaswa kulaumiwa kutokana na ongezeko la visa vya kudorora kwa maadili. “Wazazi wanapaswa kujihusisha zaidi maishani mwa wanao ili kuhakikisha kwamba wanagundua pindi wanapoanza kubadilika kitabia.”

• Shinikizo la marafiki

Utafiti kwa jina ‘The State of Kenyan youth 2018’ ulifichua kwamba hofu ya kutengwa na wenzao imewalazimisha vijana kujihusisha na masuala ya mapenzi, kabla ya ndoa, tena bila kinga.

Lakini licha ya kudorora kwa maadili kuonekana kuchangia takwimu hizi, Bw Gitonga anahoji kwamba suala la kiuchumi haliwezi kupuuzwa.

• Ukosefu wa ajira

Septemba 2018 mabadiliko ya takwimu kwa mujibu wa Mpango wa Ustawi wa Umoja wa Mataifa (UNDP) yalionyesha kwamba viwango vya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wasiozidi miaka 25 vilikuwa asilimia 26.

“Ukosefu wa ajira umewalazimisha vijana wengi kujiingiza katika mahusiano na watu waliowazidi umri kama mbinu ya kupata pesa kukidhi mahita yao,” asema.

Kwa upande wa Kemboi, alibahatika baadaye kwani alipata mhisani aliyemrejesha shuleni na kumlipia karo ambapo kwa sasa yuko chuoni. “Siri kuu ilikuwa kukubali hali yangu na kuanza matibabu mara moja,” asema.

Kinyume na Kemboi, sio watu wengi wanaokubali hali yao pindi wanapogundua kwamba wana virusi, suala ambalo Dkt Gitonga anasema limekuwa changamoto katika vita dhidi ya maradhi haya, na pia limechangia ongezeko la maambukizi ya virusi hivi, vile vile vifo vya vinavyosababishwa na Ukimwi. Kwa mujibu wa takwimu za Nacc, idadi ya maambukizi mapya ya virusi vya HIV nchini ni 44, 789.

Viwango vya maambukizi miongoni mwa wanaume ni 4.5% ikilinganishwa na maambukizi miongoni mwa wanawake ambayo ni 5.2%.

Aidha, idadi ya maambukizi mapya ya virusi vya HIV miongoni mwa watoto walio chini ya miaka 15 ni 7, 982. Vile vile, idadi ya vifo vinavyohusishwa na maradhi ya Ukimwi ni 23, 902, huku vifo vilivyohusishwa na maradhi haya miongoni mwa watoto walio chini ya miaka 15 vikiwa 4,312.

Kwa sasa Kemboi anatumia aliyopitia kuwa kama funzo la kuwapa vijana ushauri na kuhamasisha watu kuhusu Ukimwi huku akizidi kuwapa moyo wale ambao tayari wanaishi na virusi hivi.

Japo anasema kwamba kuambukizwa virusi vya HIV sio mwisho wa maisha, anasisitiza kwamba vijana hawapaswi kujihatarisha kiafya kwa kujihusisha na mapenzi kiholela hasa bila kinga ili kupata manufaa ya muda mfupi.

You can share this post!

Ukahaba ni hatia kama uavyaji mimba – Serikali

SHINA LA UHAI: Huenda ukapima ubongo wa mtoto angali tumboni

adminleo