Benki kutoza riba za juu
Na CHARLES WASONGA
WAKENYA wamejipata katika hali ya zamani ambapo benki za kibiashara zilikuwa zikiwatoza riba ya hadi asilimia 30 kwa mikopo waliochukua.
Hii ni baada ya wabunge Jumanne kushindwa kutupilia mbali pendekezo la Rais Uhuru Kenyatta la kwamba sheria ya udhibiti wa riba iondolewe.
Wakati suala hilo liliwasilishwa kupigiwa kura mwendo wa saa nane alasiri kulikuwa na wabunge 161 pekee bungeni ilhali kwa mujibu wa Katiba, kulihitajika thuluthi mbili za wabunge wote 349. Hii ina maana kuwa suala hilo lilihitajika kupigiwa kura na angalau wabunge 233.
Kwa hivyo, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi hakuamuru wabunge wapigie kura suala hilo kwa sababu hakukuwa na idadi tosha ya wabunge ukumbini.
Majuma mawili yaliyopita Rais Kenyatta alidinda kuutia saini Mswada wa Fedha na kuurejesha bunge na pendekezo kwamba kipengee kinachodhibiti riba inayotozwa na benki za kibiashara kiondolewe.
Pendekezo hilo moja kwa moja lilibatilisha kipengee cha 33 (2) (a) cha sheria za Benki na ambayo inasema kuwa benki hazifai kutoza riba ya zaidi ya asilimia nne kuzidi kiwango kilichowekwa na Benki Kuu ya Kenya ambayo huwa ni asilimia tisa.
Hii ina maana kuwa chini ya sheria hiyo, benki hazikufaa kutoza zaidi ya asilimia 13 kwa mikopo zinazotoa kwa wateja wao.
Pendekezo la Rais Kenyatta kwamba sheria hiyo iondolewe lina maana kuwa benki zitakuwa huru kutoza riba ya zaidi ya asilimia 13 kwa mikopo kama ilivyokuwa kabla ya sheria hiyo kupitishwa mnamo 2019. Hii ni baada ya mswada uliodhaminiwa na mbunge wa Kiambu Jude Njomo.
Sasa kufeli kwa wabunge kuweka kando pendekezo la Rais Kenyatta kunamaanisha kuwa Mswada huo wa Fedha, ukiwa na pendekezo hilo, sasa utawasilishwa kwake autie saini.
Hata hivyo, wabunge Jumanne waliifanyia mabadiliko machache memoranda yenye pendekezo la Rais ili kuwakinga wale ambao tayari wanalipa mikopo yao sasa wasilipe riba ya juu.
Wale ambao wataomba mikopo baada ya Rais kutia saini mswada huo wa fedha ndio watatozwa riba ya juu.
Katika memoranda aliyoiwasilisha bungeni, Rais Kenyatta alisema aliamua kuondoa sheria ya udhibiti wa riba kwani chini ya sheria hiyo benki nyingi zilikataa kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo.
Kwa upande mwingine serikali ilikuwa ikikopa kwingi kutoka kwa benki za humu nchini na hivyo kuinyima sekta ya biashara ndogo ndogo (SMEs) nafasi ya kupanuka.