Michezo

Juventus ugenini leo Jumatano kupiga na Lokomotiv

November 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MOSCOW, Urusi

MABINGWA wa Serie A, Juventus watakuwa ugenini nchini hapa leo Jumatano usiku kupepetana na Lokomotiv Moscow katika pambano la Ligi Kuu ya Ulaya.

Vijana hao wa kocha Maurizio Sarri wanaongoza kundi D kwa pointi saba wakati Lokomotiv wakijivunia pointi tatu katika nafasi ya tatu nyuma ya Atletico Madrid baada ya kujibwaga uwanjani mara tatu.

Wenyeji ambao walishindwa na Atletico nyumbani na baadaye Juventus ugenini, watahitaji kushinda mechi ya leo ili kujiongezea matumaini ya kufuzu kutoka katika kundi hili ambalo pia linajumuisha Bayern Leverkusen ya Bundesliga.

Wenyeji wangali na uwezo wa kumaliza katika nafasi ya tatu jedwalini, nafasi ambayo itawawezesha kushiriki michuano ya Eropa League, msimu ujao.

Vijana hao wa kocha Yuri Semin wataingia uwanjani baada ya mwishoni mwa wiki kutoka sare 1-1 na FC Ufa katika pambano la ligi kuu nchini hapa, wanakoshikilia nafasi ya tatu, pointi tatu tu nyuma ya vinara Zenit St Petersburg.

Hata hivyo, wameshinda tu mechi tano kati ya 14 za Ulaya jijini hapa, tatu kati ya nne kwa timu za Italia, rekodi inayowapa mashabiki wao wasiwasi mkubwa.

Juventus wanaongoza msimamo wa kundi hilo baada ya kucheza mechi tatu. Walianza kwa sare ya 2-2 na Atletico Madrid kabla kuandikisha ushindi dhidi ya Leverkusen na baadaye Lokomotiv.

Katika mkondo wa kwanza, mabao ya Juventus yalifungwa na Paulo Dybal dakika ya 77 na dakika ya 81.

Huu ni mwaka wa 20 kwa vigogo hao wa Italia kushiriki hatua ya makundi ya michauno hii, na wametinga hatua ya 16 bora kati ya 19.

Robo-fainali

Msimu uliopita, Juventus walifuzu kwa hatua ya robo-fainali, lakini kwa mshangao wakabanduliwa na Ajax Amsterdam ya Uholanzi.

Hata hivyo, klabu hiyo imepoteza fainali tano za klabu bingwa Ulaya, na hawajashinda taji hilo tangu 1996. Vilevile, nyumbani wanakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Inter Milan kwenye vita vya kuwania ubingwa wa Serie A.

Wataingia uwanjani leo baada ya ushindi finyu wa 1-0 dhidi ya Torino katika mechi ya Serie A mwishoni mwa wiki, uliowarejesha kileleni mwa jedwali, mbele ya Inter ambao kwa sasa wanaendelea kuvuma chini ya Antonio Conte aliyekuwa na Chelsea, msimu uliopita.

Kwingine, ushindi kwa Paris Saint-Germain katika mechi ya leo ya Kundi A dhidi ya Club Brugge utawawezesha kufuzu kwa hatua ya makundi kabla ya kucheza mechi mbili.

Mabingwa hao wa Ufaransa wamejikusanyia jumla ya pointi tisa na watakuwa wakicheza na Brugge ambao wanakamata nafasi ya tatu jedwalini.