• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
Raila motoni kwa ‘kuwatusi’ mabinti Wakamba

Raila motoni kwa ‘kuwatusi’ mabinti Wakamba

Na WAANDISHI WETU

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amejipata pabaya kutokana na kauli aliyotoa majuzi kuwahusu wanawake wa jamii ya Wakamba.

Bw Odinga alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa kumpigia debe mwaniaji wa ODM katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kibra, Imran Okoth mwishoni mwa wiki.

“Unajua Wakamba ni waaminifu, hasa akina mama. Wakisema wanakupatia, wanakupatia,” akasema Bw Odinga.

Kauli hiyo imewakera wengi hasa viongozi wa wanawake na kisiasa wa jamii hiyo.

Aliyekuwa mwaniaji wa ugavana katika Kaunti ya Machakos, Bi Wavinya Ndeti na Seneta wa Kitui, Bw Enoch Wambua walimshambulia Bw Odinga kutokana na walichokitaja kuwa kutoa matamshi ya kudunisha Wakamba.

“Baba (Odinga), nimeshangazwa na kauli yako. Wakamba ni waaminifu lakini hatutaki kudunishwa. Tulikuunga mkono kwa miaka 10 na jamii yetu inahitaji kuheshimiwa,” akasema Bi Ndeti.

Seneta Wambua naye alimtaka Bw Odinga kuwaomba msamaha wanawake wa jamii hiyo inayothibiti kaunti za Machakos, Makueni na Kitui.

“Ninamheshimu Raila, lakini matamshi yake hayakufaa. Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ameunga mkono Bw Odinga kwa miaka mingi lakini sasa inasikitisha kwamba sasa anadunisha jamii ya Wakamba,” akasema Bw Wambua.

“Tuko tayari kufanya muungano na watu wengine ambao wanatuheshimu. Hatuwezi kutusiwa tukiwa tumenyamaza,” akasema Seneta huyo.

Bw Wambua aliwataka wakazi wa eneobunge la Kibra wamfundishe Bw Odinga adabu kwa kukataa kumpigia kura mwaniaji wa ODM katika uchaguzi wa kesho.

Katika majengo ya Bunge, wabunge kutoka eneo la Ukambani walimtaka Bw Odinga aombe msamaha kwa jamii yao kwa ujumla.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa wa Muungano wa Wabunge wa Ukambani Bw Makali Mulu, viongozi hao walisema ikiwa Bw Odinga hataomba msamaha basi jamii hiyo itakatiza kabisa uhusiano wowote naye kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Maneno ambayo Raila alitumia kurejelea watu wa jamii yetu ni kielelezo cha matusi mabaya zaidi. Kwa hivyo, tunamtaka afafanue ikiwa aliyoyatoa yalikuwa mzaha au aombe msamaha kwetu sote kama jamii. Tunaongea hapa kwa niaba ya watu wetu kule mashinani ambao wamekerwa zaidi na matamshi yake,” akasema Bw Mulu.

Naye Bw Wambua akauliza: “Mbona Raila anawatusi Wakamba wakati ambapo alikuwa akiwaomba wale wanaoishi Kibra wampigie kura mgombeaji wa ODM? Itakuwa vipi watu ambao anawaona kama duni wasaidie chama chake kushinda katika uchaguzi huo mdogo?”

Viongozi hao waliwataja magavana watatu kutoka Ukambani: Alfred Mutua (Machakos), Charity Ngilu (Kitui) na Profesa Kivutha Kibwana (Makueni), ambao waliandamana na Bw Odinga kumpigia debe mgombeaji wa ODM kama ‘wasaliti’ na kwamba hawakuwakilisha jamii hiyo.

“Watatu hao hawakuwa wanazungumza kwa niaba ya Wakamba. Hawa na wasaliti ambao walikuwa wakiongea kwa niaba yao binafsi,” akasema Bw Mulu.

Wabunge wengine walioandamana nao ni Jessica Mbalu (Kibwezi Mashariki), Paul Nzengu (Mwingi Kasakazini), Gideon Mulyungi (Mwingi ya Kati) na Nimrod Mbai (Kitui Mashariki).

Wakati huo huo, Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi ametisha kumchukulia hatua za kisheria Bw Odinga na maafisa wa chama hicho kwa kumhusisha na kashfa ya Goldenberg.

Akijibu matamshi ya Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna kwamba alisababishia nchi hasara kupitia kashfa hiyo, Bw Mudavadi alisema viongozi wa ODM wanajua aliondolewa lawama kupitia tume kadhaa za uchunguzi.

Ripoti za ANITA CHEPKOECH, BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

You can share this post!

Taharuki UG wafuasi wa upinzani wakikamatwa

PWANI: Wanawake waombwa kukubalia waume kuoa wake wengi

adminleo