Pesa ndizo kiini cha kuvunjika kwa ndoa ya Linturi, korti yaelezwa

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi mstaafu Mzee John Langat, 87, Jumanne alieleza mahakama inayosikiza kesi ya talaka kati ya Seneta Mithika Linturi na Marrianne Kitany kwamba pesa ndizo kiini cha kuvunjika kwa ndoa hiyo.

Alisema aligonga mwamba katika jitihada za kusuluhisha mzozo baina yao wanandoa hao wawili.

“Nilidhani suala nilililoitwa kutafuta suluhu lilikuwa rahisi mbali lilikuwa nzito kwa vile lilihusu masuala ya pesa,” alisema Mzee Langat.

Babu huyo kutoka kaunti ya Kericho ambaye ni mjomba wa Marrianne, alisema kikao cha kusaka suluhu kilipoanza “suala la fedha lilichukua muda mrefu. Marrianne alidai pesa zake zote zilitumika akijenga nyumba ya kifahari ya Runda na nyingine mbili kaunti ya Meru.”

“Ati umesema suala la fedha ndilo lilichipuka,” wakili Dunstan Omari anayemwakilisha Marrianne alimwuliza Mzee Langat.

“Ndio Marrianne alitueleza Mithika alichukua hatimiliki na kujizolea mikopo mikubwa kwenye benki na alikuwa ameshindwa kuzilipa,” alijibu.

“Je, Linturi alijibu kuhusu madai hayo,” Bw Omari alimwuliza Mzee Langat.

“Hakusema chochote ila alikiri mbele ya wazazi wake kuwa atazilipa wiki iliyofuata,” hakimu mkuu Peter Gesora anayesikiza kesi hiyo alifahamishwa.

Mzee Langat alisema Marrianne aliwaeleza ametumia pesa zake zote kustawisha jumba la Runda na majumba mengine mawili kaunti ya Meru.

“Mlalamishi katika kesi hii alisema alimjengea Mithika nyumba ya kifahari Meru pamoja na ya wazazi wake,” alisema Marrianne.

Kesi inaendelea kusikizwa.