Makala

USWAHILINI: Mwanamke wa Kirabai hakuruhusiwa kupiga ngoma za kitamaduni

November 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LUDOVICK MBOGHOLI

JAMII ya Warabai ambayo ni miongoni mwa jamii nyInginezo za Kimijikenda haikuruhusu wanawake kupiga ngoma za kitamaduni wala kucheza ngoma hizo kama wafanyavyo wanaume.

Kulingana na wazee wa jamii hiyo waliotembelewa na makala haya hivi majuzi, wanawake walikubaliwa tu kuimba na kujaza sauti ya kiitikio ila kwa masharti hawafai kukaribiana na wanaume.

Wazee hao wanasema zamani za mababu zao, wanawake waliheshimiwa kwa kutekeleza tu majukumu yao ya nyumbani, lakini heshima haikuwepo kwenye tamasha za kimila, hasa kwenye shughuli za tohara ambapo ngoma za kitamaduni zilichezwa.

Inasemekana ilikuwa aibu kwa jamii kwa wanawake kujihusisha kwenye burudani zote za kitamaduni, kwani wanapokiuka marufuku hiyo wanatajwa kuwa ni wanawake wasiokuwa na heshima, hivyo hawastahili kutangamana na wenzao wanaofuata kanuni na desturi za jadi.

Familia ambayo ilimruhusu mwanamke (aliyeolewa kwenye boma) kucheza ngoma za kitamaduni, ilitajwa ni familia iliyolaanika na hivyo ilitengwa na jamii nzima.

Hata hivyo, wazee waliohojiwa na makala haya, wanadai kulingana na mapito ya nyakati, utamaduni huo ulilegezwa na kuangamia polepole hadi kufikia kikomo leo hii.

Kwa jumla, inasadikiwa wazee wa zamani ambao waliimarisha utamaduni huo, walikuwa na wakati mgumu kuweza kuafikia malengo ya kijamii kwani usasa mambo leo ulionekana kuchukua nafasi kubwa.

Kunako karne ya 15 hadi 17, mabadiliko makubwa yalibainika huku mila na desturi za mababu wa Kirabai zikisambaratishwa na hisia kali za mfumko wa kanuni mpya za kitamaduni.

‘Si ruhusa kwa wanawake’

Kuna baadhi ya shughuli ambazo wanawake wa Kirabai hawakuruhusiwa kushiriki. Kwa mfano, kukwea juu ya minazi, miembe na miti mingineyo ya matunda, sawa na kupiga ngoma au kucheza sambamba na wanaume wao au wavulana vijijini.

Inasadikiwa ilikuwa ni hali au jambo la aibu lililotamausha vijiji, kwa mwanamke wa boma kutangamana ngomani au kushiriki na wanaume kucheza na kuimba nyimbo za kitamaduni.

Mila ilikataa kabisa msimamo wa kisasa na kushikilia msimamo wa mababu wa jadi ulioambatanishwa na matambiko ya kimbari.

Licha ya yote hayo, siku hizi mambo yamebadilika pakubwa kwani wanawake hushirikiana na waume wao ngomani, hasa kwenye sherehe za harusi, kitaifa, au mialiko ya matamasha ya kitamaduni.