• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
Washukiwa wa mauaji ya Kasisi Kyengo kushtakiwa Embu mnamo Novemba 11

Washukiwa wa mauaji ya Kasisi Kyengo kushtakiwa Embu mnamo Novemba 11

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA watatu wa mauaji ya Kasisi Michael Maingi Kyengo watashtakiwa kwa mauaji Jumatatu wiki ijayo katika Mahakama Kuu ya Embu.

Hakimu mkazi katika mahakama ya Milimani, Paul Mayova ameamuru Jumanne kwamba polisi wanafaa kuwapeleka washukiwa hao kujibu mashtaka ya mauaji mbele ya Jaji wa MahaFkama Kuu katika Kaunti ya Embu.

Bw Mayova ametoa agizo hilo baada ya kuombwa na kiongozi wa mashtaka ya umma awaruhusu maafisa wa polisi wawahoji washukiwa hao watatu kwa siku moja hadi Alhamisi ndipo wafunguliwe shtaka la mauaji.

“Kuna washukiwa watatu waliotiwa nguvuni kufuatia kifo cha Kasisi Kyengo aliyetoweka na maiti yake ikapatikana imezikwa katika ufuo wa mto Kaunti ya Embu,” Bw Mayova alielezwa.

Hakimu alielezwa mshtakiwa polisi wanaochunguza kesi hiyo wamebakisha sehemu kidogo kukamilisha uchunguzi huo.

“Afisa anayechunguza kesi hii atasafiri hadi Embu kesho (Alhamisi) kukamilisha mahojiano na mashahidi kisha awafungulie washukiwa mashtaka katika mahakama kuu Embu,” mahakama imeambiwa.

Kiongozi huyo wa mashtaka amemweleza hakimu washukiwa wote: Michael Mutunga, Mwangangi Kavivya na Solomon Mutava watashtakiwa pamoja.

“Mutunga, Kavivya na Mutava watashtakiwa pamoja kwa mauaji ya Kasisi Michael Maingi Kyengo,” Bw Mayova amefahamishwa.

Naye amewauliza swali washukiwa.

“Je mnapinga ombi mzuiliwe kwa siku moja zaidi kumwezesha afisa anayechunguza kesi dhidi yenu kusafiri hadi Embu kukamilisha uchunguzi?” Bw Mayova amewauliza washukiwa.

Wamesema hawapingi.

Mahakama imeamuru washukiwa hao wazuiliwe hadi Alhamisi kumwezesha mkurugenzi wa mashtaka ya umma kuwafunguliwa mashtaka.

“Polisi watawasafirisha hadi Embu ambapo mtajibu shtaka la kumuua Kasisi Michael Kyengo,” Bw Mayova amewaeleza washtakiwa.

Hakimu ameamuru washukiwa hao wazuiliwe hadi Novemba 11, 2019, watakapojibu shtaka la mauaji katika mahakama kuu ya Embu.

Wakili anayewatetea washukiwa hao hakupinga ombi hilo la kuwazuilia kwa siku moja ndipo ofisi ya DPP iwafungulie mashtaka.

Mmoja wa washukiwa hao, Kavivya, wiki iliyopita alisimulia mbele ya hakimu mwandamizi Hellen Onkwani jinsi Kasisi Kyengo alivyouawa kinyama na maiti yake kuzikwa kando ya mto.

Kavivya ameungama ni yeye alimfunga Kasisi Kyengo mikono na miguu akiwa uchi wa mnyama kisha wakamuua.

Mshukiwa huyo alikiri alilipwa Sh1,500 kumsaidia Mutunga kumuua aliyesema “ walikuwa wanamtoa kafara.”

Hakufafanua ilikuwa kafara ya nini.

Kasisi Kyengo alikuwa amefungiwa ndani ya buti la gari la Mutunga.

Kasisi Kyengo alikuwa akihudumu katika kanisa la katoliki la Thatha kaunti ya Machakos.

Mara ya mwisho ya kuonekana akiwa hai ilikuwa Oktoba 8 2019 katika soko la Kaewa akiendesha gari lake.

  • Tags

You can share this post!

Seneti yapitisha pendekezo serikali iruhusiwe kukopa hadi...

IEBC yasema saini za kuvunjilia mbali Kaunti ya Taita...

adminleo