• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
IEBC yasema saini za kuvunjilia mbali Kaunti ya Taita Taveta ziko sawa

IEBC yasema saini za kuvunjilia mbali Kaunti ya Taita Taveta ziko sawa

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta sasa yuko huru kuendelea na mchakato wa kuvunjilia mbali Kaunti ya Taita Taveta baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuthibitisha Jumatano kwamba saini zilizowasilishwa na Gavana Granton Samboja ni sahihi.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amesema kuwa kati ya saini 39,300 zilizowasilishwa 21,861 hazikuwa na dosari.

Majina ya watu 7,073 ambao walitia saini, hayako katika sajili ya wapigakura na wengine 3,686 walitia saini zaidi ya mara moja.

Watu 5,899 waliotia saini katika vitabu hivyo si wapigakura katika Kaunti ya Taita Taveta.

Saini za watu 781 zilikataliwa kwa sababu hazikuwa na nambari ya kitambulisho cha taifa au hawakutia alama yoyote katika sehemu au kijisanduku cha kutia saini.

Kaunti ya Taita Taveta ina wapigakura 180,000 hivyo Gavana Samboja alihitaji saini za watu 18,000 pekee kuanzisha mchakato wa kuvunjilia mbali kaunti hiyo.

“Hii ni kufahamisha washikadau pamoja na umma kwamba saini za Taita Taveta zimetimiza idadi inayohitajika kuanzisha mchakato wa kuivunjilia mbali,” akasema Bw Chebukati.

Rais Kenyatta sasa atabuni jopokazi ambalo litasikiliza pande husika; upande wa Gavana Samboja aliyekusanya saini hizo na upande wa madiwani pamoja na washikadau wengineo.

Jopokazi hilo baadaye litawasilisha mapendekezo yake kwa Rais Kenyatta ambaye atatoa uamuzi wake wa mwisho kuhusu hatima ya Kaunti ya Taita Taveta.

Iwapo Rais Kenyatta ataivunjilia mbali basi Kaunti ya Taita Taveta itakuwa chini ya usimamizi wa serikali ya kitaifa huku tume ya IEBC ikiandaa uchaguzi mpya wa gavana na madiwani.

Gavana Samboja alianza mchakato wa kutaka kuvunjilia mbali Kaunti ya Taita Taveta baada ya kutofautiana na madiwani kuhusu bajeti ya Sh5.6 bilioni ya mwaka wa matumizi ya fedha wa 2019/2020.

Upunguzaji bajeti

Gavana Samboja alishutumu madiwani kwa kupunguza bajeti ya serikali ya kaunti.

Madiwani walijitetea kwamba walipunguza bajeti hiyo kwa sababu serikali ya kaunti imekuwa ikitumia Sh270 milioni kulipa wafanyakazi vibarua 1,600.

Lakini Bw Samboja anasisitiza kuwa wafanyakazi wanaodaiwa kuwa vibarua ni wauguzi na walimu wa shule ya chekechea.

Tume ya IEBC ilipokea vitabu vya saini kutoka kwa afisi ya rais aliyeitaka kuthibitisha saini kabla ya kubuni jopokazi.

Gavana Samboja anaungwa mkono na wabunge kutoka Taita Taveta ambao hivi majuzi walisema kuwa hatima ya kaunti hiyo sasa iko mikononi mwa Rais Kenyatta.

Iwapo Rais Kenyatta atavunjilia mbali kaunti hiyo itakuwa ya kwanza kuvunja tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi.

Mnamo 2015, Rais Kenyatta alitupilia mbali pendekezo la jopokazi lililoongozwa na Mohammed Nyaoga kumtaka kuvunjilia mbali Kaunti ya Makueni. Rais Kenyatta alishauri pande zilizokuwa zikizozana kutumia njia mbadala kusuluhisha tofauti baina yao.

You can share this post!

Washukiwa wa mauaji ya Kasisi Kyengo kushtakiwa Embu mnamo...

AKILIMALI: Ukakamavu wake katika ufugaji wa kuku umeendelea...

adminleo