Makala

MBURU: Viongozi watakao wakazi wazaane wamejaa ubinafsi

November 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

MATOKEO ya sensa yaliyotolewa na serikali wiki hii yameanika hila za baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini tena, ambao wamekuwa wakiwapotosha wananchi kuwa na familia kubwa, hata bila kujali uwezo wao wa kukimu mahitaji yao.

Punde baada ya Shirika la Takwimu Kitaifa (KNBS) kutangaza matokeo ya hesabu ya watu iliyofanywa Agosti, jambo kuu ambalo viongozi wengi wamekuwa wakilalamikia ni kuwa, idadi ya watu ambao kaunti zao zilitangazwa kuwa nao ni ndogo mno.

Viongozi hawa wamelalamika kuwa haiwezekani kuwa wakazi wa maeneo yao wameongezeka kwa kiwango kidogo tangu matokeo ya sensa ya miaka kumi iliyopita mnamo 2009, wengi wao wakipinga uhalali wa matokeo hayo.

Cha kushangaza ni kuwa, viongozi waliojitokeza kulalamika hadi sasa ni wale maeneo yao yalikuwa na wakazi wachache. La kustaajabisha ni kwamba, hakuna yeyote aliyejitokeza kufikia sasa, kulalamika kuwa wakazi wa eneo lake ni wengi kupita kiasi.

Hakuna kiongozi ambaye ameshauri wakazi wa eneo lake kuwa na idadi ya watoto wanaoweza kulea bila changamoto za kiuchumi.

Lakini kinaya ni kwamba, kuna baadhi yao wengine ambao hata wamejitokeza kuwahimiza wakazi wao kutoshiriki mbinu za upangaji uzazi, ili wawe na watoto wengi, kuongeza idadi yao wakati wa sensa.

Ni ubinafsi ulioje kwa kiongozi kuwashauri watu kujifungua watoto wengi kwa ajili ya sensa na kuongeza idadi ya kura pekee, bila kujali jinsi mahitaji ya kila siku ya watoto hao yatakidhiwa wala mazingira watakamoishi.

Vilevile, hila kubwa kwa viongozi- ambao wana familia ndogo licha ya mapato yao makubwa inaonyesha jinsi viongozi wetu bado hawajali maslahi ya wananchi, ila kila mara wao husukuma ajenda zitakazowanufaisha tu na kuwakweza kisiasa.

Miaka ya nyuma, taifa lilishuhudia matukio ya kutamausha, ambapo viongozi walijitokeza wazi kusifia hali ya watu kujifungua watoto wengi, wakati wengi wa wanaopotoshwa hivi huwa ni maskini wasio na mapato.

La kuudhi zaidi ni kuwa, viongozi wa kike pia wamekuwa wakihusika katika upotoshaji huu wa watu, licha ya kuwa ndio wanatarajiwa kuwa mstari wa mbele kushauri kina mama na wazazi kwa jumla, kujifungua watoto ambao wana uwezo wa kuwalea na kuwasomesha ipasavyo.