Rais anavyovuruga vita dhidi ya ufisadi
Na VALENTINE OBARA
MVUTANO kati ya Idara ya Mahakama na Afisi ya Rais umeibua shaka kuhusu kujitolea kwa utawala wa Jubilee kupambana na ufisadi.
Hii inatokana na kuwa mahakama zina wajibu mkubwa katika vita dhidi ya ufisadi kwani ndizo zinatoa adhabu kwa washukiwa baada ya kusikiza ushahidi kutoka kwa idara zingine kama vile polisi na Idara ya Mashtaka ya Umma (DPP).
Mnamo Jumatatu, Jaji Mkuu David Maraga alilalamika vikali kuhusu jinsi Serikali Kuu inavyohujumu mahakama akisema hatua hiyo inalemaza utendakazi wake hasa vita dhidi ya ufisadi.
Hii ni baada ya idara yake kupunguziwa bajeti na Wizara ya Fedha wiki chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukataa kuidhinisha majaji 41 walioteuliwa na Tume ya Huduma za Majaji (JSC) akidai wengi ni watovu wa maadili.
Hatua za Rais Kenyatta dhidi ya mahakama zinatoa jumbe za kukanganya, moja ikiwa amekuwa akitangaza kujitolea kukomesha ufisadi nchini na pili ni kuwa utawala wake unadhoofisha kimakusudi moja ya idara zinazopasa kufanikisha vita hivyo.
Mnamo Jumatatu, Jaji Maraga alionya kwamba mojawapo ya athari za serikali kupunguzia Mahakama fedha ni kwamba kesi za ufisadi hazitakamilika haraka: “Mikakati tuliyoweka kukamilisha kesi za ufisadi haraka sasa imekwama,” akasema.
Kulingana naye, kesi za ufisadi huhitaji umakinifu kwa vile kuna stakabadhi chungu nzima zinazowasilishwa kortini kwa wakati mmoja, washtakiwa na mashahidi ni wengi pamoja na mawakili ambao kila mmoja wao hutaka kusikizwa, hivyo kuna haja ya kuwepo kwa majaji wa kutosha kufanya kazi hiyo
“Kama vile nimewahi kusema awali, hatuwezi kukubali Mahakama ilaumiwe bila sababu na hivyo basi madai kwamba Mahakama ndiyo imezembea kati ya asasi zote zinazopambana na ufisadi si kweli kamwe,” akaeleza.
Mwezi uliopita, Mkurugenzi wa DPP, Bw Noordin Haji alikiri hali ni ngumu katika juhudi zao za kuwashtaki washukiwa na kuendesha kesi za ufisadi akitaja moja ya matatizo kuwa uhaba wa majaji.
Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli alisema kulemaza Mahakama wakati huu ni hatua isiyofaa.
“Rais alipotangaza msimamo wake kupambana na ufisadi kisheria, jukumu la Mahakama lilikuwa wazi. Mahakama pekee ndiyo inaweza kutenda haki kwa msingi wa ushahidi unaotolewa,” mratibu wa muungano wa mashirika ua umma, Bw Suba Churchil akasema.