• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Hali ngumu wanayopitia baadhi ya wauzaji wa nguo

Hali ngumu wanayopitia baadhi ya wauzaji wa nguo

Na SAMMY WAWERU

BI Peninah Wairimu anauza nguo kwa muda wa zaidi ya miaka saba sasa.

Anasema aliamua kufanya biashara hii baada ya kuchoshwa na kazi za ofisi.

Uamuzi huo, anasema, ulichochewa na shinikizo za pale kazini.

“Mshahara ulikuwa mdogo, hivyo basi nilitafuta njia mbadala kutafuta mapato na biashara ikanikubali,” anasema Peninah.

Kulingana na mfanyabiashara huyo, baina ya 2012 na 2017, uwekezaji katika sekta ya biashara ulinoga na mapato yalikuwa maradufu ya mshahara aliolipwa.

Peninah 32, huuza nguo za watoto hasa marinda, suruali ndefu na sweta. Vilevile, huuza nguo za wanawake na mavazi ya ndani ya wanaume, miongoni mwa bidhaa zingine.

Malalamiko yamekuwepo miongoni mwa wafanyabiashara kwa kupanda kwa uchumi, unaosababisha hali ngumu ya maisha. Hali hiyo ni bayana katika kibanda cha Peninah Wairimu kilichoko eneo la Guthurai 45, Kiambu.

Kulingana na mfanyabiashara huyo ambaye ni mama wa watoto wawili, siku inapita au kuisha bila kufanya mauzo, jambo linalomtia kiwewe. “Si ajabu siku mbili au tatu kufanya mauzo ya Sh200 pekee. Kodi ya nyumba, chakula na karo, gharama zote hizo zinanisubiri,” akaambia Taifa Leo.

Hata ingawa hajutii uamuzi wake kugura ajira aliofanya awali, Peninah anasema biashara zimezorota kwa kile kinatajwa kama uchumi kuwa ghali. Ushuru wa juu unaotozwa, ni baadhi ya vichangio vya uchumi kuyumba.

“Ushuru unapaswa kutozwa kiasi kuwa wanaoulipia hawatalemewa na gharama wanayotundikwa mgongoni. Mzigo ukiwa mzito, anayeubeba atachoka,” apendekeza Dennis Muchiri, mchanganuzi wa masuala ya biashara na uchumi.

Kibanda cha Peninah awali kilikuwa mithili ya ghala la nguo, lakini sasa hali si hali tena. Bidhaa zake huzinunua katika soko maarufu la Gikomba, lililoko jijini Nairobi, na wafanyabiashara humo pia wanapitia hali ngumu. “Tunanunua beli bei ghali, hivyo basi tunalazimika kugawana gharama hiyo na wateja wetu,” aeleza Mama Shiro, muuzaji wa kijumla.

Mfanyabiashara Peninah anasema yeye pamoja na wafanyabiashara wenza wanajaribu kukwepa nguo ghali ili kudumisha wateja, hatua anayotaja inawapa kipindi kigumu.

Mama huyo ana vibanda viwili, eneo la Githurai na Kahawa Wendani, na kwamba vyote vinapitia changamoto hizo.

Mwishoni na mwanzoni mwa kila mwezi, mauzo huwa ya juu lakini wakati huu wafanyabiashara wamechengwa. “Kwa kuwa tunaelekea msimu wa Krismasi, matumaini yetu ni kuwa biashara zitaimarika na serikali isikie kilio chetu,” anasema, kauli yake ikitiliwa mkazo na Zipporah Ndereba.

“Ninauza mavazi mahususi kwa jinsia ya kike, na biashara imekuwa ikidorora,” anasema Zipporah.

Alazimika kuacha

Samuel Gitau anasema kuwa mwaka 2017 alilazimika kuacha uuzaji wa nguo na badala yake akaanza huduma za M-Pesa, kufuatia hali ngumu ya kunawiri kwa biashara.

“Nguo zinaenda na msimu, na huziuza shamrashamra za Krismasi zinabisha hodi,” anasema.

Ili kuimarisha biashara, wahusika wanashauriwa kupanua mawazo yao ambapo wanahimizwa kutumia mitandao kama vile Facebook, Instagram na WhatsApp kutafuta wateja zaidi.

Teknolojia inaimarika, na badala ya watu kuzunguka sokoni, wanatumia mitandao ya kijamii kuagiza bidhaa ambazo wanapelekewa hadi ama nyumbani au ofisini.

Kuna programu za simu ambazo zimebuniwa kwa shughuli hiyo, pamoja na makundi ya biashara mitandaoni.

Hata hivyo, unashauriwa kuwa makini kwa sababu matapeli pia wamesheheni.

You can share this post!

BAMBIKA: Bae mpya ninaye, ila mimba ndiyo kidogo bado

Wahalifu wawaua maafisa wawili wa polisi Kayole

adminleo