• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Rais aonya maafisa wanaochangia kuendelea kuwepo kwa visa vya ukeketaji wasichana

Rais aonya maafisa wanaochangia kuendelea kuwepo kwa visa vya ukeketaji wasichana

Na SAMMY WAWERU

ONYO kali limetolewa kwa maafisa wa serikali wanaoendeleza kwa njia moja au nyingine vitendo vya ukeketaji wa wasichana nchini.

Rais Uhuru Kenyatta amesema Ijumaa hatua kali kisheria zitachukuliwa kwa maafisa watakaopatikana na hatia.

Akizungumza katika mkutano na wadau wanaojituma katika vita dhidi ya ukeketaji yakiwemo mashirika ya kijamii katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi, kiongozi wa taifa amewahakikishia kuwa idara za usawa wa jinsia, elimu, afya na usalama, zitashirikiana nao katika suala hilo.

“Mkiona chifu au naibu chifu anayeongoza sherehe za ukeketaji muniambie, mtaona vile nitamfanyia,” amesema Rais Kenyatta.

Rais pia ameahidi kushirikisha viongozi wa mataifa jirani ili kupiga jeki vita dhidi ya ukeketaji.

Ameeleza jitihada zake katika kutetea nafasi ya kina mama katika jamii, akisema “nafasi yao si jikoni pekee”.

“Nafasi ya akina mama nchini ipo. Mambo ya kudhulumu wanawake tumeyakataa,” amesema.

Akisisitiza kuhusu ukeketaji, amesema wazee na utamaduni wa Waafrika ni masuala yanayoheshimiwa, ila kuna mambo yaliyopitwa na wakati “tunayopaswa kuacha hususan unyanyasaji wa kijinsia.”

Rais ameeleza imani yake kwamba kufikia 2022 ukeketaji wa wasichana, FGM, utakua umefikia kikomo.

Baadhi ya jamii nchini zimekuwa zikiendeshwa shughuli hiyo haramu kisiri. Kuna wahusika waliojipata kuandamwa na sheria, hasa wanaoendesha kitendo hicho na vilevile wanaokubali kukeketwa.

Kauli ya Rais Kenyatta kuhusu jinsia pia imejiri wakati ambapo baadhi ya kina mama viongozi wanafanya mchakato wa uafikiaji wa kipengele cha thuluthi mbili, cha usawa wa jinsia.

Inasemekana mjadala huo pia umejadiliwa katika mapendekezo ya BBI. Aidha, BBI ni tume maalum iliyobuniwa kuangazia masuala ibuka kufuatia salamu za maridhiano baina ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga Machi 2018, maarufu kama Handshake.

You can share this post!

Gavana Joho alazwa akiugua Malaria

Rais atakiwa aingilie kati kunusuru sekta ya majanichai

adminleo