Changamoto zinazohusu vipande vya ardhi zatatuliwa Ruiru

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Ruiru wamepata afueni baada ya kliniki ya kutatua shida za mashamba kukamilika Jumatano.

Afisi ya ardhi ya mji wa Ruiru imekuwa na shughuli nyingi kwa muda wa miezi mitatu mfululizo ili kutatua baadhi ya matatizo na changamoto wanazopata wakazi hao.

Afisa mkuu wa ardhi katika ofisi ya Ruiru Bw Robert Mugendi alisema zaidi ya watu 30,000 walileta shida zao katika ofisi hiyo ili ziweze kutatuliwa.

“Tumefanya kazi ya ziada ili kufikia kiwango hicho kwa sababu mara nyingi tulikuwa tukiingia kazini mapema saa mbili hadi saa moja za jioni. Nashukuru wenzangu katika ofisi hii ambao tulifanya kazi kwa pamoja,” alisema Bw Mugendi.

Alisema walilazimika kupitia vyeti vyote na stakabadhi za watu hao ili kuthibitisha iwapo kulikuwa na utata ili zirekebishwe.

Alizidi kueleza kuwa ofisi hiyo mpya iliyofunguliwa imekuwa ni afueni kwa wakazi wa Ruiru ambao kwa muda mrefu walisafiri mwendo mrefu hadi Thika au Kiambu ili kutafuta huduma.

“Tutahakikisha kila mmoja aliye na shida inayohusu kipande cha ardhi anapata haki yake ipasavyo kwa kukabidhwa cheti kinachomfaa cha ardhi yake. Tunataka kuona Ruiru inapunguza shida za kukosa vyeti vya kumiliki mashamba,” alisema afisa huyo.

Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara alipongeza jinsi shughuli hivyo ilivyoendeshwa kwa njia ya uwazi bila yeyote kuitishwa hongo ili ahudumiwe.

“Mimi mbunge wa hapa Ruiru nililazimika kuzungumza na Wizara ya Ardhi kuzuru mji huu ili watatue shida hizo za muda mrefu,” alisema Bw King’ara.

Alisema kazi iliyofanyika kwa muda wa miezi mitatu mfululizo ni ya kupongezwa kwa sababu kila mmoja ameelezwa matatizo yake kuhusu ardhi yake na pia wana imani kubwa ya kupokea hatimiliki hivi karibuni.

Mmoja wa wahusika katika shughuli hilo Bi Grace Njoroge alisema kazi waliyofanya kwa muda huo wote ni ya kuridhisha kwa sababu waliweza kuwahudumia wakazi kutoka maeneo 11 katika kaunti ndogo ya Ruiru.

“Kazi yetu muhimu ilikuwa ni kuwasajili wote waliokuwa na shida; baadaye tuliwasaidsia kujaza fomu muhimu kabla ya kuwatuma ofisini zikaguliwe rasmi kama ziko sawa,” alisema Bi Njoroge.

Hata hivyo alisema baadhi ya vyeti vilivyokuwa na kesi mahakamani pia vitashughulikiwa ipasavyo na kuhakikisha kila kitu kinakamilika.

Habari zinazohusiana na hii