MUTUA: Demokrasia iko hatarini eneo la Afrika Mashariki
Na DOUGLAS MUTUA
MAMBO yakienda yanavyoonekana katika ukanda wa Afrika Mashariki, huenda Kenya ikabaki taifa pekee lenye sura ya demokrasia.
Hata hili sina hakika nalo kwani wajuao wamedai huenda mradi wa maridhiano, almaarufu BBI, unanuiwa kubadilisha Katiba ili Rais Uhuru Kenyatta anate madarakani.
Matukio mawili muhimu yametokea hivi majuzi katika ukanda huu na kunisadikisha kuwa bado tuko mbali sana na demokrasia, hatujakubali kujitawala kikamilifu.
Ile kasumba ya kutamani kukaliwa mguu wa kausha na bwana mkubwa tuliyorithishwa na mkoloni ingali nasi, tuko radhi kuongozwa kiimla badala ya kujiamulia mambo.
Ulionishtua ni mwibuko wa kesi ya ajabu jijini Dar es Salaam. Mtu anataka sheria inayomtaka rais atawale kwa mihula isiyozidi miwili, iondolewe ili Rais John Magufuli aitawale Tanzania milele.
Hoja kuu ya Bw Dezydelius Patrick Mgoya ni kwamba Rais Magufuli ni mchapa kazi sana, akiondoka baada ya kipindi cha pili – ambacho bado hajapata – mambo yatakwenda tenge.
Wewe nami tunajua mambo yanavyokwenda wakuu wakitaka kitu katika nchi hizi zetu zilizoitwa mashimo ya mavi na Rais Donald Trump wa Amerika kwa kuzidisha utepetevu.
Huenda mshtaki Mgoya ni kikaragosi tu anayetumiwa na Rais Magufuli pamoja na watu wanaotaka dikteta huyo anate madarakani. Labda wamemfadhili kuwasilisha kesi hiyo mahakamani wakilenga mbali sana, mbele ya muda anaotarajiwa kustaafu.
Lengo la aliyemfadhili Bw Mgoya, ikiwa kwa hakika alifadhiliwa, halihusiani na Uchaguzi Mkuu ujao wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika mwakani, la hasha!
Huo, hata asipofanya kampeni, Rais Magufuli anajua atashinda kwa haki au vinginevyo kwani Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho jogoo liwikalo na kuwanyamazisha wote.
Labda Magufuli na wasaidizi wake hawataki aondoke madarakani kama anavyotarajiwa kikatiba ifikapo 2025.
Unaweza kujiuliza ni nani ambaye angetaka Magufuli, mkali wa kuwavaa wala rushwa, adumu madarakani kwa muda usiojulikana ikiwa ni mzalendo wa kweli.
Hapa hakuna suala la uzalendo, ni watu wajanja kuandaa mikakati ya kuipora nchi siku za baadaye kwa manufaa yao binafsi.
Wazoefu wa masuala ya kisiasa watakwambia kiongozi wa hulka ya ukali kama Magufuli huwa na pupa ya kufanya mambo kwa utendeti ili kujizolea sifa lukuki kabla ya kustaafu. Akijua hastaafu, eti ataondolewa hapo na kifo, basi ataketi kitako na kula mali yake akijidanganya amekwisha weka mikakati tosha ya kuitawala nchi kutoka ikulu.
Kiongozi akianza kustarehe na kusinzia kochini, wanaomzingira huingia shughulini kuipora nchi na kufanya maovu mengineyo wakijua fika wa kulaumiwa yumo ikulu.
Walioishi miaka ya kwanza ya utawala wa Daniel Moi watakwambia alikuwa na kila dalili ya kuwa kiongozi bora Afrika ikiwa si dunia nzima – mnyenyekevu na mpole.
Alipokipasha joto kigoda cha ikulu kikampendeza kikweli, waliibuka watu wasiokuwa na vyeo vyovyote maalumu wakatuhangaisha kwa miaka 24 tusijue kwa kutorokea!
Magufuli, ikiwa ni mwerevu anavyodai, anapaswa kukataa vishawishi vyovyote vile vya kumdumisha madarakani.
Si kwa manufaa yake, Watanzania wala Afrika Mashariki.
Inatabirika kwamba huenda mahakama, ambazo zinamwogopa ajabu, zikaamua suala la ukomo wa vipindi lipigiwe kura bungeni au kwenye kura ya maamuzi.
Ana satua ya kukubali au kukataa, uamuzi ambao utawasaidia au kuwadhuru zaidi wanyonge wa ukanda huu wanaopania kupanua demokrasia, ambayo iko hatarini.
Nilisubiri kwa hamu na ghamu, kwa jumla ya miezi sita, kuona serikali ya umoja wa kitaifa ikiundwa nchini Sudan Kusini mwezi huu lakini wapi! Wadau wangali wanaliliana maini.
Rais Salva Kiir na mpinzani wake mkuu, Dkt Riek Machar, wameshindwa kupatana kabisa, hali ambayo imewaacha wapatanishi wao wakijikuna vichwa na kuuliza itakuwaje.
Si kwema; Paul Kagame wa Rwanda ataachia madaraka baada ya 2039 nao Yoweri Museveni wa Uganda na Pierre Nkurunziza wa Burundi hawajasema watang’atuka lini. Tuna shida.