Makala

FUNGUKA: ‘Hutaamini ninavyohifadhi kumbukumbu ya nimpendaye!’

November 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

NI kweli kwamba mapenzi ni kikohozi, na endapo maradhi haya yatakukumba basi itakuwa vigumu kuficha hisia zako.

Gongo, 45, raia wa taifa moja bara Ulaya anawakilisha wanaume ambao maradhi haya yamewaduwaza kiasi cha kwamba inakuwa vigumu kufikiria.

Yeye ni mfanyabiashara ambapo kwa viwango vya kawaida, hali yake ya kifedha sio mbaya sana. Kwa hivyo kimapato yuko thabiti, huku uzuri wake kimaumbile pia ukimpiga jeki na kumweka katika nafasi nzuri ya kuvutifa macho ya mabinti popote anapopita.

Lakini uzuri huu usikuduwaze kwani maisha ya kisiri ya kaka huyu ni ya kustaajabisha.

“Miaka miwili iliyopita nilimpoteza mke wangu baada ya kuugua kwa muda mfupi. Ni suala lililoniacha na huzuni kiasi cha kwamba kwa mwaka mmoja, singeweza zungumza wala kujihusisha na yeyote.

Aidha, msiba huo uliniathiri kiasi cha kwamba ilinibidi nibuni mbinu ya kiajabu kuhifadhi kumbukumbu ya marehemu mke wangu.

Badala ya kuuzika mwili wake, nimeuhifadhi nyumbani kwangu. Mwili wake uko katika kijichumba kidogo ambacho ni sehemu ya chumba changu cha kulala.

Kijichumba hicho kimejaa kumbukumbu za mke wangu ikiwa ni pamoja na picha, mavazi na viatu alivyopenda kuvalia. Vibeti alivyopenda kubeba, na hata vipodozi alivyokuwa akitumia. Aidha, kuna maua ambayo lazima yabadilishwe kila baada ya wiki moja.

Ili kuuhifadhi mwili wake, kila wiki namlipa daktari wa maiti kumdunga dawa ya kuchangamsha seli za mwili, bidhaa ambayo hasa hutumika katika mochari kuhifadhi maiti. Mwili huu umekalishwa kwenye kiti alichokuwa akipenda akiwa hai, na hivyo unapoingia mle na kukutana naye, ni rahisi kudhani kwamba ni mtu aliye hai.

Kila siku lazima maiti ya bibi yangu ioshwe, kupakwa mafuta, kupodolewa na kubadilishwa nguo. Aidha, mimi humlipa mwanasaluni kumletea wigi za kisasa kila mwezi.

Ikiwa unataka kuwa mpenzi, mchumba au mke wangu hatimaye, lazima nikufahamishe kuhusu marehemu mke wangu na hata kukutambulisha kwake.

Sio hayo tu, lazima uwe tayari kuchukua jukumu la kumshughulikia marehemu mke wangu kwa kumuosha, kumpaka mafuta na kumpamba. Aidha, lazima uwe tayari kumkubali kama mke mwenza.

Pia, kila mara lazima uwe unamtembelea chumbani mwake, huku ukitenga angakau siku moja kwa wiki kukaa naye siku nzima chumbani mwake mchana kutwa.

Mbali na hayo, kutokana na sababu kuwa pamoja na mke wangu bado hatukuwa tumejaliwa watoto, basi lazima ukubali kwamba tutakapojaliwa watoto watapewa majina kutoka kwetu na kwa akina marehemu mke wangu. Endapo hauko tayari kufuata masharti haya basi una uhuru wa kushika njia yako.

Sio wengi wanaojua kuhusu maisha yangu, lakini kwa familia na marafiki wa karibu, wanajua na kunielewa, japo wanahofia kwamba itakuwa vigumu kumpata mke atakayekubali haya.

Pengine wewe unajiuliza kwa nini nafanya hivyo? Nilimpenda mke wangu sana na alipofariki niliishiwa na nguvu na singeweza kufanya chochote. Hisia za kumpoteza zilinifanya nife ganzi.