Makala

DINI: Watu wanapokutazama husema wewe ni Mkristo wa aina gani, mtoaji ama mlaji?

November 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na FAUSTIN KAMUGISHA

MKRISTO hapaswi kuwa anayeambiwa juu ya Yesu, bali anayemjua Yesu binafsi; anamtambua Yesu, anamtembelea Yesu, anakutana na Yesu.

Ni katika msingi huu Yesu aliuliza, “Akawaambia, nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” (Mt 16: 15).

Je, wewe ni Mkristo anayemjua Yesu au anayejua habari juu ya Yesu?

Pilato alipomuuliza Yesu kama ni Mfalme wa Wayahudi, Yesu alimuuliza, “Unasema hivi kwa nafsi yako, au ni watu wengine waliokupa habari yangu?” (Yohana 18: 34).

Mtume Petro alikiri imani yake kwa Yesu, “Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Ni katika imani hii ambapo kanisa la Kristo limejengwa; si juu ya mwamba usio na moyo, au mwamba vuguvugu.

“Na ninyi mwasema kuwa mimi ni nani?”: ni swali la msingi katika imani ya kikristo. Laweza kutafsiriwa kama ifuatavyo: Ninyi, Waafrika, mwasema kuwa mimi ni nani?

Tunaalikwa kujibu swali hili kwa kadiri ya utamaduni wetu, na nafasi ya Injili kwa utamaduni huo.

Swali alilouliza Yesu: “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?”, linaweza kuelekezwa kwetu pia. Watu wanasema wewe ni Mkristu wa aina gani?

Kuna aina mbalimbali za Wakristo. Kuna wanaoitwa “Nguzo”. Hawa huja kanisani kila siku na kutoa sadaka. Kuna wakristo “Wachangiaji”. Hawa ni wale ambao hutoa pesa kama tu wanampenda mchungaji, na mwekahazina anayetunza pesa hizo.

Kuna wakristo wanaitwa “Waegemeaji”. Wanafanya kazi lakini hawatoi chochote. Kunao ambao ni “Watu wa Kila mwaka”. Huja kanisani wakati tu wa misimu muhimu kama vile Krismasi na Pasaka.

Kuna Wakristo wanaitwa “Watu wa pekee”. Wanasaidia na kutoa kila mara. Kisha kuna Wakristo “Sponji”. Hawa wanachukua baraka zote na kufurahia huduma wanazopewa kanisani lakini hawasaidii katika chochote.

Kuna Wakristo wanafahamika kama “Watembezi”. Wanatangatanga kutoka Kanisa hili na kwenda lingine, bila kusaidia kwa lolote. Kuna Wakristo “Wambea”. Hawa wanapenda sana chuchuchu, kusengenya watu wote isipokuwa Yesu Kristo.

Kuna Wakristo wanaitwa “Yatima”. Wanawatuma watoto wao kanisani kusali lakini wao wazazi hawaandamani nao.

Kuna Wakristo “Wanafiki”. Hawa ndio wale ambao hukataa kwenda kanisani, eti kwa sababu kuna wanafiki katika nyumba ya Mungu.

Je, watu wakikutazama wanasema wewe ni nani? Yesu hakuuliza Mafarisayo na wanasheria swali hilo. Hakugeukia Makuhani na Walawi kutaka kujua watu wanamsemaje.

Alitaka kujua kauli ya watu wa kawaida. Mafarisayo na wanasheria walimsema Yesu kumwa ni mlafi, kwa sababu alikula na kunywa na watoza ushuru.

Mafarisayo hao na wanasheria walidai Yesu anatoa watu pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebub, mkuu wa pepo wabaya.

Licha ya kusemwa hayo, Yesu alizidi kuimarika. Yesu alikutana na watu wenye machungu, wazushi na wafitini ili kuwakomboa kutoka kwa minyororo iliyokuwa imewafunga. Tukumbuke kuwa, katika historia ya dunia hakujawahi kujengwa mnara wa kuenzi wazushi, waongo, makahaba na wafitini.

Kama watu walimsema Kristo, sembuse wewe. Mtu akiwa mkarimu watu watamsema eti anajitangaza. Asipokuwa mkarimu watasema ana gundi kwenye vidole, ni mnyimi, ni bahili.

Mtu akitoa hotuba fupi sana, wanasema hakujiandaa. Akitoa hotuba ndefu, eti hazingatii muda.

Akiwa mtoto mchanga wanasema ni malaika. Akiwa mtu mzima wanasema achana na yule shetani.

Akiwa mcha Mungu wanasema ni Mkatoliki zaidi ya Papa. Asipokuwa mcha Mungu wanasema shetani amemweka mfukoni. Watu watakusema tu.