TAHARIRI: KEBS ibaini hatari kwa muda ufaao

NA MHARIRI

KWA mara nyingine, serikali imepatikana ikisinzia wakati Wakenya wakikodolea macho athari za magonjwa hatari kupitia vyakula wanavyouziwa.

Imekuwa desturi idara mbalimbali za serikali zinazotegemewa kusimamia masuala ya usalama wa umma kimaisha na kiafya kuzembea katika majukumu yao.

Iwe ni usalama kutokana na uhalifu, magonjwa, makazi duni au hata usafiri barabarani, utakuta kwamba hakuna hatua zozote mwafaka ambazo huchukuliwa hadi wakati wananchi wakishaathirika.

Hivi sasa, tunaona Idara ya Kukagua Ubora wa Bidhaa Kenya (KEBS) ikijitokeza kutoa onyo kwa umma kuhusu aina za unga wa mahindi zinazodaiwa kuwa na sumu.

Hizi ni bidhaa ambazo zimekuwa katika maduka yetu kwa muda mrefu, zikatumiwa na umma muda huo wote kisha sasa tunaambiwa huenda afya ya waliotumia bidhaa hizo zimo hatarini kwa vile unga una sumu hatari ya aflatoxin.

Ingekuwa rahisi kusifu KEBS kwa hatua iliyochukua, kama haingetokea siku moja kabla habari za kiupelelezi kupeperushwa kuhusu vyakula hatari vinavyojumuisha unga wa mahindi.

Miezi michache iliyopita, hali sawa na hii ilishuhudiwa wakati vyombo vya habari vilipofichua jinsi baadhi ya wafanyabiashara hupaka rangi nyekundu kwa nyama ili kufanya ionekane ni bidhaa ambayo haijadumu sana dukani.

Ni sharti maafisa wanaosimamia idara muhimu serikalini kama vile KEBS wafahamu kwamba wamepewa jukumu kubwa la kulinda maisha ya wananchi.

Mojawapo ya majukumu ya wanahabari ni kufichua maovu yanayotendeka katika jamii. Wakati mwingi, ufichuzi huu hufanywa kwa matumaini kwamba asasi husika zitabadili mienendo na kuimarisha utendakazi wao kwa manufaa ya wananchi.

Inavyoonekana, hali sivyo katika KEBS. Inaonekana maafisa wa idara hii wameamua kuendelea kuzembea kazini, wakifanya kazi zao jinsi ile ile ya zamani bila kujali athari ya mienendo hii.

Katika enzi hii ambapo magonjwa sugu yanatatiza binadamu ulimwenguni kote, haistahili idara muhimu kama hii ifanye kazi zake kiholela na kuchukua hatua tu baada ya watu kuathirika badala ya kuzuia athari hizo kama inavyohitajika kwa majukumu yake.

Idara kama hizi zinafaa zifanyiwe msasa wa kina kutambua changamoto iko wapi, na kama ni wasimamizi wamezembea, kuna Wakenya wengi wenye uwezo wa kutumikia umma ipasavyo.