Habari

Wabunge wataka kiini halisi cha kifo cha mwanafunzi wa Alliance kifichuliwe

April 3rd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wawili Jumanne walitaka uchunguzi wa kina ufanywe kubaini chanzo cha kifo cha mwanafunzi mmoja wa Shule ya Upili ya Alliance kilichotokea Ijumaa huku wakishuku kuwa huenda alifariki kutokana na utepetevu wa asasi zilizomshughulikia.

Wabunge hao, Johana Ng’eno (Emurua Dikkir) na Alfred Keter (Nandi Hills) walisema Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Wizara ya Elimu sharti ziendeshe uchunguzi wa kina kubaini kilichosababisha kifo cha Haroun Kipng’eno Kemboi.

“Kifo cha mvulana huyo kimezingirwa na utata. Huenda hali hii ilichangiwa na utepetevu kwa upande za usimamizi wa shule sawa na hali ilivyokuwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta,” akasema Bw Keter ambaye amekuwa akimlipia mwanafunzi huyo karo kwa sababu anatoka familia maskini.

Picha ya mwendazake Haroun Kipng’eno Kemboi wakati wa misa  ya wafu iliyofanyika katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance Aprili 3, 2018. Picha/ Anthony Omuya

Wabunge hao pia walitaka Kamati ya Bunge kuhusu Elimu kufanya uchunguzi wake huru kubaini chanzo cha kifo hicho.

Kulingana na wabunge hao, wanafunzi ambao walikuwa pamoja na Kemboi saa chache kabla ya kifo chake, waliamriwa kutozungumza.

“Hiki ni kisa kibaya zaidi kuwahi kutokea katika shule ya upili ya Alliance, ni mvulana kutoka familia masikini kutoka eneo bunge langu,” akasema Bw Keter.

 

Uchochole

Wakati mmoja Kemboi, aliangaziwa katika makala maalum katika runinga moja nchini akielezea namna alivyotengeneza mizinga ya nyuzi na kuuza ili kupata pesa za kujilipia karo kwa sababu mamake hakuweza kumudu mzigo huo.

Kifo cha Haroun Kipng’eno Kemboi kilimshtua mno mwanfunzi huyu wakati wa misa ya wafu Aprili 3, 2018 katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance. Picha/ Anthony Omuya

Wabunge hao wamewasilisha matakwa yao huku Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Kiambu Ali Abdikadir akisema maafisa kutoka Wizara ya Elimu watazuru shule hiyo kuchunguza kifo cha mwanafunzi huyo.

Hata hivyo, maelezo ya usimamizi wa shule hiyo kwamba mwanafunzi huyo alifariki kutokana na ugonjwa wa kifuo kikuu yalipuuziliwa mbali ya wabunge hao wakisema hayana mashiko.

Inadaiwa kuwa marehemu alikimbizwa katika zahanati ya shule hiyo baada ya kupata shida za kiafya.

Wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance wakati wa misa ya wafu Aprili 3, 2018  kufuatia kifo cha Haroun Kipng’eno Kemboi. Picha/ Anthony Omuya

Kuficha ukweli

“Mtu anawezaje kufariki kutokana na kifua kikuu baada ya siku mbili? Huu sio ugonjwa ambao huua haraka,” akasema Bw Ng’eno akiongeza “kile tunachoambiwa ni njama ya kuficha chanzo halisi cha kifo hiki”.

“Tunataka kujua kilichotokea na kwa nini usimamizi wa shule ulifeli kumsaidia mwanafunzi huyo haraka.”

Familia ya Kemboi inadai kuwa haikupewa maelezo kamili kuhusu kilichokuwa kikimsibu mpendwa wao hapo awali lakini baadaye wanaelezwa kwamba alifariki kutokana na kifua kikuu.

Wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Alliance waonekana kuhuzunika wakati wa misa ya wafu Aprili 3, 2018  kufuatia kifo cha Haroun Kipng’eno Kemboi. Picha/ Anthony Omuya

“Tulielezwa kuwa mwanafunzi huyo alikuwa amelazwa katika zahanati moja mjini Kikuyu Jumatatu wiki iliyopita a akafanyiwa uchunguzi Jumatano.

Lakini mnamo Ijumaa tuliarifiwa kuwa hali yake ilikuwa mbaya na baada ya dakika 15 tukapigiwa simu kwamba amefariki,” mmoja wa jamaa zake, ambaye hakutaka kutajwa jina, aliwaambia wanahabari.

Kisa hicho kinajiri mwaka mmoja baada ya aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kusimamishwa kazi baada ya visa vya wanafunzi wa kidato cha kwanza kudhulumiwa na wenzao kufichuliwa na vyombo vya habari.