• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
WANDERI: Kenya itahatarisha mustakabali wake ikiendelea kukopa

WANDERI: Kenya itahatarisha mustakabali wake ikiendelea kukopa

Na WANDERI KAMAU

MATAMSHI ya mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini) kwamba hali ya kiuchumi nchini imedorora kuliko inavyoelezwa na serikali, inapaswa kutufungua macho kuhusu mustakabali wa kiuchumi wa Kenya.

Kulingana na Bw Kuria, Kamati ya Bunge Kuhusu Bajeti imekuwa ikiwadanganya Wakenya kuhusu deni ambalo Kenya inadaiwa na nchi za nje kwa miaka saba ambayo amekuwa mwanachama wa kamati hiyo.

Alikiri kwamba taarifa za kifedha ambazo kamati hiyo imekuwa ikitoa si za kweli, ila lengo lake kuu limekuwa “kuzifurahisha asasi zingine za serikali” hasa afisi ya Rais.

Bila shaka, kauli ya Bw Kuria inafichua uhalisia mchungu ambao unapaswa kumtia kiwewe kila Mkenya kuhusu usalama wa nchi hii kutokana na madeni inayodaiwa na nchi za nje.

Kulingana na takwimu zilizopo, Kenya inadaiwa kuwa na deni la Sh5.8 trilioni. Hili linajumuisha madeni inayodaiwa na asasi za kifedha za nje kama Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo Barani Afrika (AFDB), nchi kama Uchina, Amerika, Japan kati ya wafadhili wake wengine.

Serikali vilevile inadaiwa na baadhi ya mashirika ya kifedha nchini kama vile benki na baadhi ya mashirika ya kibinafsi.

Kinachoshtua ni kwamba, hizi ni taarifa ambazo zimetolewa na serikali, hivyo, si wazi ikiwa huu ndio ukweli kuhusu deni ambalo Kenya inadaiwa.

Wiki iliyopita, Bunge la Kitaifa na Seneti zilipitisha hoja ya kuongeza uwezo wa Kenya kukopa hadi Sh9 trilioni. Hili linanaamisha kwamba Serikali ya Jubilee haijakoma kukopa….Hali hii itaendelea!

Maswali yanaibuka: Je, mustakabali wa Kenya u salama? Huenda tunajiweka katika hatari ya kutekwa na nchi zile zingine ikiwa tutashindwa kulipa madeni yao? Ukweli ni upi kuhusu hali ya kiuchumi nchini?

Kila wakati anapotetea hatua ya serikali kuendelea kukopa mikopo mikubwa mikubwa kutoka nje, Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akitaja sababu kuu kuwa ufadhili wa miundomsingi muhimu kama barabara.

Hata hivyo, huwa anasisitiza kuwa Kenya haijapitisha kiwango ambacho inapaswa kukopa.

Ilipofikia sasa, ni lazima serikali ieleze ukweli kamili kuhusu hali ya uchumi nchini.

Ni kinaya kwa serikali kufadhili miradi ya maendeleo wakati wananchi wake wanaendelea kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha. Je, huenda Kenya ikawa koloni tena ili kulipa madeni ya kimataifa?

[email protected]

You can share this post!

WANDERI: Wakenya watasalia watumwa daima dahari

NGILA: Ujio wa Amazon utaboresha uwekezaji mitandaoni

adminleo