• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
NGILA: Yafaa ujielimishe mwenyewe kuhusu sarafu za dijitali

NGILA: Yafaa ujielimishe mwenyewe kuhusu sarafu za dijitali

Na FAUSTINE NGILA

WAKATI mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda alipojitia kitanzi mwezi uliopita baada ya kupoteza Sh500,000 katika kipochi cha dijitali, pengo kubwa lililopo katika ukosefu wa maarifa kuhusu sarafu za dijitali lilianikwa.

Sarafu za dijitali zimekumbwa na utatanishi, ugumu wa kuelewa na mfumuko wa thamani yake usioweza kubashiriwa. Lakini watu wanaendelea kuwekeza katika majukwaa haya bila kupata elimu inayohitajika.

Tatizo kuu la vijana wa Afrika ni kwamba wanalenga kuitwa mabwanyenye katika kipindi cha muda mfupi, na ndio maana wanawekeza pesa bila kuelewa mbinu bora ya kufanya hivyo.

Ripoti ya Citibank inaonyesha kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yanayomiliki idadi kubwa ya sarafu za dijitali.

Nilipomtembelea Bi Beatrice Wanjiru katika mkahawa wake mjini Nyeri ambao unakubali malipo ya sarafu za dijitali kama Bitcoin, Bitcoin Cash na Dash, niling’amua kuwa vijana wa mashinani wanaamini Bitcoin ni aina ya chakula katika mkahawa huo.

Alikiri kuwa kwa wakati mmoja, pia yeye alipoteza Bitcoin za thamani ya Sh500,000 kwenye tukio la wizi mtandaoni.

Ni kutokana na wizi huu ambapo benki kuu za Kenya, Uganda, Tanzania, Malawi, Zimbabwe, Nigeria na Afrika Kusini zimewaonya raia wao dhidi ya kuwekeza katika sarafu hizi kwa kuwa “hakuna usalama wowote mitandaoni na majukwaa hayo hayajadhibitiwa na serikali.”

Nikimhoji afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Amerika Paxful inayoeneza elimu ya sarafu hizi duniani Bw Ray Youssef, alisema ni hatua nzuri kwa mataifa hayo kutahadharisha raia dhidi ya kuwekeza kwenye biashara wasiyoielewa.

Ni wazi kuwa wakati wafanyabiashara wa mitandaoni wanapoteza hela zao kutokana na udukuzi, serikali hupatwa na hofu.

Hata hivyo, watu wengi wanaopoteza fedha zao ni wale wazembe wasiopenda kusoma wala kutafiti kuhusu jambo baada ya kulisikia.

Haufai kuisubiri serikali ikuelimishe kuhusu masuala ambayo ishatoa tahadhari, jielimishe mwenyewe kwa kuomba ushauri wa wataalamu.

Kukosa kufanya hivi kutakuletea balaa. Usiwasikie wenzio wakisema mfumo huo hauwezi kudukuliwa, chukua muda wako na kutafiti ni kwa nini watu wengi Amerika wamepoteza hata mabilioni kutokana na wizi aina hii.

You can share this post!

Wanawake Kilifi lawamani kukataza waume kupanga uzazi

Wazee walia kunyimwa hela za uzeeni

adminleo