• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
WASONGA: Fujo za Kibra ni aibu kwa ODM na viongozi wake

WASONGA: Fujo za Kibra ni aibu kwa ODM na viongozi wake

Na CHARLES WASONGA

UCHAGUZI mdogo wa kuwania kiti cha ubunge cha Kibra ulikamilika Ijumaa iliyopita baada ya mgombeaji wa ODM Benard Otieno Okoth ‘Imran’ kutangazwa mshindi.

Na inaridhisha kuwa mpinzani mkuu wa Bw Imran, McDonald Mariga alimpigia simu na kuungama kushindwa, hata kabla ya matokeo kutoka vituo vyote 183 vya kupigia kura kuthibitishwa.

Lakini hali ilikuwa tofauti wakati wa upigaji kura kwani fujo zilishuhudiwa sehemu kadha katika eneo bunge hilo.

Watu kadhaa walishambuliwa na makundi ya vijana kwa madai kuwa walikuwa wakiwahonga wapiga kura ili waunge mkono mgombeaji fulani.

Viongozi kama vile Aaron Cheruiyot (Seneta wa Kericho), Vincent Musyoka (Mbunge wa Mwala), Nelson Koech (Belgut), Rigathi Gachagua (Mathira), Didmus Baraza, Silvanus Osoro (Mugirango Kusini) na Bony Khalwale walivamiwa na kufurushwa kutoka vituo mbalimbali vya kupigia kura na wahuni hao hao.

Kinachoudhi ni kwamba maafisa wa polisi hawakuchukua hatua zozote kuzuia matukio kama haya. Walionekana wakitizama tu huku wahuni wakiwahangaisha wanasiasa wa chama cha Jubilee.

Na hadi jana idara ya Polisi haikuwa imetoa taarifa zozote kuhusiana na fujo zilizoshuhudiwa Kibra siku ya Alhamisi.Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Kibra, Lucas Ogaro alisema afisi yake haijapokea malalamishi kutoka kwa yeyote huku Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DDP) Nordin Haji akiahidi kuwa wahusika watachukuliwa hatua “baada ya polisi kukamilisha uchunguzi wao”.

Wale waliozua fujo Kibra wanafaa kutambua kuwa kila Mkenya ana haki ya kufanya maamuzi ya kisiasa bila kuzuiawa na yeyote.

Na kwa mujibu wa kipengee cha 38 (2) (C) cha Katiba ya sasa haki hiyo inajumuisha kuunga mkono chama chochote cha kisiasa na wagombeaji wake katika chaguzi mbalimbali.

Kwa hivyo, fujo za Kibra zichunguzwe na wahusika wakamatwe na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria ili iwe funzo kwa wenye nia kama hiyo siku zijazo, haswa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Nadhani ni fujo hizo zilizochangia idadi ndogo ya wapigakura waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo mdogo.Ikiwa juzi tuliona Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa na mlinzi wake walikamatwa kuhusiana na fujo zilizotokea katika wadi wa Ganda siku moja kabla ya uchaguzi mdogo, hatua sawa na hiyo inapasa kuchukuliwa dhidi ya waliochochea fujo Kibra.

Kinaya ni kwamba ghasia za Kibra zinatokea katika ngome ya kisiasa ya kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye, pamoja na Rais Uhuru Kenyatta walibuni muafaka wa maridhiano ya kisiasa, maarufu kama handisheki kwa lengo la kukomesha visa kama hivyo.Isitoshe, fujo hizo zinajiri wakati ambapo Wakenya wanasubiri ripoti iliyotayarishwa na jopo la maridhiano (BBI).

Wajibu mkuu wa jopo hilo ulikuwa ni kutoa mwongozo kuhusu namna ya kukomesha fujo kabla, wakati na baada ya chaguzi humu nchini.

You can share this post!

WATU NA KAZI ZAO: Ukakamavu umemwezesha kujiimarisha licha...

TAHARIRI: Pia tuangalie faida za kongamano hili

adminleo