Rais wa zamani wa Amerika alazwa ili kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu
Na AFP
WASHINGTON D.C., AMERIKA
ALIYEKUWA Rais wa Amerika Jimmy Carter alilazwa Jumatatu katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Emory, Atlanta kufanyiwa matibabu ya kupunguza shinikizo la ubongo kutokana na kuvuja damu baaada ya kuanguka mara kadha hivi majuzi.
Kulingana na taarifa kutoka kwa kituo cha Carter Center, Carter alipangiwa kufanyiwa upasuaji huo leo Jumanne asubuhi, ikiongeza kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 95 alikuwa “akipumzika vizuri” na mkewe, Rosalynn, alikuwa pamoja naye.
Hakuna habari zozote zilizotolewa kuhusiana na hali iliyosababisha Rais huyo wa zamani kulazwa hospitalini.
Mnamo Oktoba, Carter alilazwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Emory wiki tatu baada ya kuugua jeraha dogo kwenye nyonga alipoanguka nyumbani kwake Plains, Georgia.
Aliruhusiwa kurejea nyumbani kutoka hospitalini siku chache baada ya ajali hiyo.
Kisa cha awali cha kuanguka Oktoba, kilihitaji Carter kushonwa uso lakini akarejea kazini punde baada ya matibabu hayo kwa mradi wa ujenzi wa makao kwa kundi lisilo la kiserikali la Habitat for Humanity.
Mnamo Mei, Rais huyo wa zamani wa chama cha Democratic alivunja fupaja lake akiwa nyumbani kwake vilevile na kuhitajika kufanyiwa upasuaji.
Alilazwa hospitalini kwa muda mfupi mnamo 2017 kwa kukosa maji mwilini na akapatikana na saratani ya ngozi mnamo 2015.
Carter, aliyewahi kuwa mkulima wa njugu na gavana wa Georgia, alimshinda Rais wa Republican Gerald Ford mnamo 1976 na kuibuka Rais wa 39 Amerika, ambapo alihudumu kipindi kimoja cha miaka minne katika White House.
Urais wake uligubikwa na kudorora kwa uchumi, mtanziko wa kawi na utekaji wa mateka wa Amerika na Iran, lakini pia alichangia pakubwa katika kufanikisha Mkataba wa Camp David uliowezesha maafikiano ya amani kati ya Misri na Israeli.
Alibwagwa katika uwaniaji wake kwa mara ya pili mnamo 1980 na mgombea wa Republican Ronald Reagan.
Baada ya kubanduka ofisini 1981, Carter aliendelea na kuwa mwanaharakati tajika wa haki za kibinadamu.
Alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2002 kwa juhudi zake katika kupata suluhu za amani kwa machafuko kimataifa, kuendeleza demokrasia na haki za kibinadamu, kukuza maendeleo kiuchumi na kijamii.
Carter pamoja na mkewe walibuni Carter Center mnamo 1982 ili kuendeleza kazi yao ya kimataifa na utetezi wa haki za kibinadamu.