• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
GWIJI WA WIKI: David N. Wachira

GWIJI WA WIKI: David N. Wachira

Na CHRIS ADUNGO

HUWEZI kabisa kuyafikia mengi ya malengo yako iwapo hujiamini maishani.

Ukweli na ujasiri ni nguzo muhimu katika mafanikio ya mtu.

Usiruhusu mawazo yoyote yasiyo na sifa hizi akilini mwako. Jifunze kutokata tamaa, kuwa mtu mwenye msimamo kisha penda kwenda na wakati.

Kufaulu katika jambo lolote ni zao la jitihada, nidhamu na uvumilivu. Thamini kile unachokifanya huku ukijitahidi kuwa mbunifu. Jitolee kuongozwa na mapenzi ya dhati katika chochote unachokitenda huku ukipania kujiimarisha kwa kujiwekea malengo mapya ya mara kwa mara.

Huu ndio ushauri wa Bw David Ndegwa Wachira – mwandishi na mwalimu wa Kiswahili Katika Shule ya Upili ya Starehe Boys’ Centre, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Ndegwa alizaliwa katika eneo la Pumwani, Nairobi akiwa mtoto wa tatu katika familia ya watoto sita wa Bi Mary Nyambura na marehemu Peter Wachira. Baada ya kujipatia elimu ya awali katika Shule ya Msingi ya Ontulili, Meru kati ya 1975 na 1981, alijiunga na Shule ya Upili ya Starehe Boys’ Centre mnamo 1982. Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCE) mnamo 1985 na kuendeleza elimu yake ya kiwango cha ‘A-Levels’ shuleni Starehe Boys’ Centre kati ya 1986 na 1987. Alijiunga na Shirika la Kitaifa la Huduma kwa Vijana (NYS), Gilgil mwanzoni mwa 1988 kwa kipindi cha miezi mitatu kabla ya kupata kibarua cha kufundisha Kiswahili na Jiografia katika Shule ya Upili ya City High, Nairobi.

Japo wazazi walikuwa tayari wamepanda mbegu za mapenzi ya Kiswahili ndani ya Ndegwa wakati alipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi, ni Bw Kinuthia aliyekuwa mwalimu wake wa Kiswahili shuleni Starehe Boys’ Centre ndiye aliichochea pakubwa ilhamu yake. “Msukumo wa kukichangamkia Kiswahili ulianza nilipokuwa mwanafunzi wa Kidato cha Tano. Natambua upekee wa mchango wa Bw Kinuthia katika kunielekeza vilivyo na kunitia katika mkondo wa nidhamu kali.”

USOMI

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton kusomea Isimu, Kiswahili na Jiografia mnamo 1988. Anakiri kwamba kariha ya kuzamia utetezi wa Kiswahili ni zao la kutangamana na wahadhiri wake chuoni, hasa Profesa Hezron Mogambi na marehemu Profesa Profesa Jay Kitsao ambaye hadi kufariki kwake alikuwa Mwenyekiti wa Idara ya Isimu, Lugha na Fasihi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Wengine waliomchochea pakubwa kitaaluma ni Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Profesa Kithaka wa Mberia, Profesa Chacha Nyaigotti Chacha na Profesa Kitula King’ei wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairobi.

“Kwa kutangamana na watu wa nui hiyo, ambao walikipenda na kukithamini sana Kiswahili, nilipata motisha na ujasiri wa kukichapukia Kiswahili kwa usanifu mkubwa ajabu.”

UALIMU

Baada ya kufuzu na kuhitimu mnamo 1991, alianza kufundisha Kiswahili na Kiingereza katika Shule ya Upili ya Thunguma, Nyeri alikoamsha ari ya kuthaminiwa kwa masomo ya lugha miongoni mwa wanafunzi.

“Wanafunzi walianza kushiriki kwa ari zaidi mashindano ya uigizaji na kughani mashairi katika tamasha za kitaifa za muziki na drama, jambo lililoinua pakubwa viwango vya wa- nafunzi katika masomo ya lugha.”

Alihamia Shule ya Upili ya Kiamariga, Nyeri mnamo 1992 kisha kuelekea Giakaibei High, Nyeri alikohudumu kwa miaka miwili hadi mwishoni mwa 1994. Alijiunga na Starehe Boys’ Centre & School mnamo 1995 akiwa afisa msaidizi wa mwasisi na mkurugenzi wa kwanza wa shule hiyo, marehemu Dkt Geoffrey William Griffin.

Katika wadhifa wake, Ndegwa alishughulikia uteuzi wa wanafunzi waliotokea katika familia zisizojiweza kwa minajili ya kudhaminiwa shuleni Starehe Boys’ Centre na katika vyuo vikuu vya kigeni vikiwemo Pennsylvania na Massachusetts vya USA kupitia mradi wa Overseas University Placement.

Mwenyekiti wa zamani wa Jopo la Kiswahili shuleni Starehe Boys’ Centre, Bw Simon Wanda (Oxford, Uingereza) na aliyekuwa Mbunge wa Kibra marehemu Ken Okoth (St Lawrence, USA) ni miongoni mwa zaidi ya wanafunzi 100 waliosaidiwa na Ndegwa kujiunga na vyuo vikuu vya kifahari barani Ulaya na Marekani.

Mwishoni mwa 1995, alianza kufundisha na kuaminiwa ulezi wa Chama cha Kiswahili (kwa sasa Jopo la Kiswahili) shuleni Starehe Boys’ Centre miezi michache baadaye.

Kupitia Jopo, wanafunzi wana jukwaa mwafaka la kukuza vipaji vyao katika uandishi, uigizaji, ulumbi na utunzi wa mashairi. Mbali na kuwapa wanachama fursa ya kuzamia ipasavyo mada mbalimbali zinazowatatiza madarasani, Jopo pia huchapisha Jarida la Mwangaza na kuandaa makongamano ya Kiswahili.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea stashahada baada ya digrii ya kwanza (PGDE) kati ya 1998 na 1999. Msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ulimchochea kurejea chuoni Kenyatta mnamo 2011 kusomea shahada ya Uzamili katika taaluma ya Ushauri na Saikolojia. Alifuzu mwishoni mwa 2013.

Ndegwa anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili inayoongozwa kwa sasa na Bi Damaris Manzi shuleni Starehe Boys’ Centre ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaoujivunia kila mwaka matokeo ya KCSE yanapotolewa.

Ndegwa ana tajriba pevu katika usahihishaji wa mitihani ya kitaifa ya KCSE. Amekuwa mtahini wa Karatasi ya Tatu ya KCSE Kiswahili chini ya Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC) tangu 2002. Anajivunia kuandaa na kuhudhuria makongamano mbalimbali katika sehemu nyingi za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

UANDISHI

Anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza rasmi tangu akiwa wanafunzi. Nyingi za insha alizozitunga zilimvunia tuzo za haiba kubwa katika ngazi za shule ya msingi, sekondari na chuo kikuu. Baada ya kuandika ‘Nuru ya Isimujamii’, ‘Maandalizi Mufti’ na ‘Marudio Kamili ya KCSE’ mnamo 2006, kampuni ya Moran ilimchapishia msururu wa vitabu vya ‘Breakthrough Workbook Kiswahili’ kati ya 2010 na 2013. Mbali na kutunga miongozo ya vitabu vingi vya fasihi, anajivunia kutafsiri makala mbalimbali ya Shirikisho la Kenya la Wakulima wa Kiafrika (KFAP) kati ya 2007 na 2012.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kudumisha uhai wa ndoto za kuwa mhadhiri wa chuo kikuu, Ndegwa ambaye pia ni mkulima maarufu viungani mwa miji ya Meru na Kerugoya anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu wanaoshikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali.

Kwa pamoja na mkewe Bi Florence Wambui ambaye ni mwandishi, mtahini wa kitaifa na mwalimu wa somo la Dini shuleni Starehe Boys’ Centre, Ndegwa amejaliwa watoto watatu: Holiness, Faith na Oliver.

Azma yake kubwa ni kuzidi kuwa balozi na mtetezi wa Kiswahili na kuhakikisha anashirikiana na weledi wengine wa lugha hii ashirafu ili kudumisha hadhi ya kote duniani.

You can share this post!

Moto usiku wasababisha taharuki Mombasa Hospital

KINA CHA FIKIRA: Chipukizi wenye raghba ya kuandika...

adminleo