Habari Mseto

Watahiniwa 34 waandamwa na vituko KCSE ikiendelea

November 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WAANDISHI WETU

VISA vya kadhaa vimekumba Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) katika eneo la Nyanza huku watahiniwa 34 wakiathirika.

Katika Kaunti ya Kisii, mtahiniwa mmoja katika Shule ya Upili ya Bunyonge, eneo la Bomachoge Chache alifanyia mtihani wake katika Kituo cha Polisi cha Ogembo baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuavya mimba mnamo wikendi.

Katika Kaunti ya Kisumu, mwanafunzi katika Shule ya Upili ya St Peter’s Kajulu alilazwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kombewa mnamo Ijumaa baada ya gesi aina ya Xylene kumlipukia usoni mwake.

Katibu wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) katika kaunti hiyo Bw Zablon Anangwe alisema kuwa shule za upili la Kasagam na ile ya Wasichana ya St Theresa pia zilikumbwa na matatizo ya gesi hiyo hatari.

Naye msichana wa miaka 17 aliyekamatwa anadaiwa kuavya mimba ya miezi sita Jumatano iliyopita.

Kijusi cha mtoto huyo kilipatikana kimewekwa katika karatasi ya plastiki na kutupwa katika mto ulio karibu.

Katika kisa kingine, watahiniwa 14 katika Shule ya Upili ya Kenyoro PAG katika eneo la Marani waliagizwa wawe wakifika shuleni humo kutoka majumbani mwao kufanya mitihani baada ya kupatikana wakivuta bangi.

Vile vile, walimpiga naibu mwalimu mkuu. Wanafunzi hao walikuwa wakilala katika bweni la shule hiyo.

Ripoti za Benson Ayienda, Elizabeth Ojina na Justus Ochieng’