WATU NA KAZI ZAO: Hutengeneza breki za tuktuk
Na SAMMY WAWERU
VIJIGARI vyenye magurudumu matatu maarufu kama tuktuk viliingia nchini chini ya utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki na vimesaidia pakubwa katika ubunifu wa ajira.
Ukizuru miji kama vile Mombasa ambao ni ngome yavyo, Nairobi, Kisumu, Nakuru na mitaa kadhaa Kiambu vimesheheni.
Mbali na kusaidia kutatua suala la ajira, tuktuk zimerahisisha shughuli za usafiri.
Ada yake, nauli, ni nafuu ikilinganishwa na ya bodaboda – huduma zinatolewa kupitia pikipiki.
Mtaa wa Mwihoko, Mumbi, Progressive na Githurai 45, iliyoko Kaunti ya Kiambu, vijigari hivyo vimeajiri mamia ya vijana. Kila dakika hutakosa kuvitazama vikisafirisha abiria na hata mizigo.
Hakuna kitu kilichotengenezwa na binadamu kinachokosa kuharibika, hivyo basi kinahitaji fundi wa kukikarabati.
Bw Michael Waweru ni mtaalamu wa breki za tuktuk na kazi hiyo ameifanya kwa zaidi ya miaka saba.
“Nilisomea huduma za tuktuk na kukarabati breki nikiwa Mombasa, ambapo viliingia kwa mara ya kwanza,” asema mekanika huyo.
Amekuwa Kiambu kwa takriban miaka mitatu tangu atoke Pwani.
Kulingana na mekanika huyo, ni gange isiyokosa riziki kukimu familia yake.
Bw Waweru anasema malipo hutegemea tatizo au matatizo ya gari, akidokeza kwamba hayapungui Sh100 kwa kila analorekebisha. “Msimu wa mvua, kazi huwa imenoga,” akasema katika gareji yake iliyoko mtaa wa Mumbi, Kaunti ya Kiambu.
Sawa na magari mengine, breki za tuktuk zimesindikwa kwenye bakuli maalum lililounganishwa na rimu ya tairi, ingawa zake ni za nyuma. Gurumu la mbele na ambalo ni moja halina breki, ni la kuongoza na hudhibitiwa kwa usukani unaowiana na wa pikipiki.
Breki za tuktuk hudhibitiwa kwa kukanyaga sawa na magari mengine. Nyaya zimeunganishwa hadi kwenye bakuli ili kutekeleza shughuli hiyo.
Klachi ya tuktuk iko kwenye usukani, na kwa kawaida hutumika katika ubalidilishaji wa gia.
Aidha, bakuli lina laini za breki maarufu kama ‘linings’ ambazo hubadilishwa zinapoisha.
“Zinahitaji kubadilishwa kwa umakinifu kwa kuwa ndizo hudhibiti kasi ya tuktuk,” anaelezea mekanika Waweru.
Kila gurudumu lina laini mbilimbili za breki, hivyo basi kwa jumla ni nne. Kulingana na Bw Waweru moja hubadilishwa kwa Sh200.
Hakuna kazi isiyokosa changamoto, fundi huyo anaiambia Taifa Leo kwamba kombe zilizozeeka kupindukia hutatiza kubadilisha hivyo basi laini huisha upesi. “Baadhi ya wateja hulalamika hazikutengenezwa ipasavyo. Shida huendelea kujiri ikiwa bakuli imezeeka na kuisha,” anasisitiza.
Huduma za tuktuk eneo hilo ziliasisiwa na kuanzishwa mnamo 2014. Zinaongozwa na muungano wa Githurai Tuktuk Association (GTA) chini ya mwenyekiti wake Bw Peter Kinyua.
“Sekta ya vijigari hivi ni mojawapo ya inayosaidia kuimarisha uchumi wa eneobunge la Ruiru na Kiambu kwa jumla,” akasema Bw Kinyua wakati wa mahojiano. Aidha, mitaa ya Mumbi, Mwihoko, Progressive na Githurai ina zaidi ya tuktuk 300.