Mfanyabiashara akamatwa katika kesi ya Cohen
Na RICHARD MUNGUTI
MSEMO wa Wahenga kwamba hakuna msiba usioandamana na mwenziwe ulitimia Jumanne wakati mshukiwa wa mauaji ya bwanyenye Tob Cohen, Peter Karanja alipokamatwa kushtakiwa kwa wizi wa mabavu baada ya kuunganishwa kwa kesi ya mauaji na Sarah Wairimu Kamotho.
Naam Karanja aliingilia lango kuu la mahakama lakini akiondoka “alipitisha katika tundu lililo katika seli za mahakama kuu na kuigizwa ndani ya gari la Subaru na kufufulilizwa moja kwa moja hadi Gilgil kujibu shataka la wizi wa mabavu.”
Karanja alikamatwa punde tu alipotoka mbele ya Jaji Stellah Mutuku aliyeunganisha kesi dhidi yake na Sarah.
Kila mmoja alikuwa ameshtakiwa peke yake kwa mauaji ya Cohen na upande wa mashtaka ukaomba kesi hiyo iunganishwe.
Baada ya kutoa uamuzi , wakili anayemtetea Karanja alisimama na kueleza mahakama kwamba kuna maafisa wa polisi wanaosubiri kumtia nguvuni mshtakiwa.
“Naomba hii mahakama ifahamu maisha ya Karanja yamo hatarini baada ya kuonywa na afisa anayesimamia kituo cha Polisi cha Gilgil Albert Kipchumba,” Jaji Mutuku alifahamishwa.
Karanja alidai afisa huyo alimtisha kwamba atajuta endapo atarudi mjini Gilgil.
Jaji Mutuku alifahamishwa , polisi watamfungulia shtaka la wizi wa mabavu.
Ilidaiwa Karanja alivunja makazi ya Mbunge wa Gilgil Bi Martha Wangari.
Jaji Mutuku alifahamishwa makazi hayo yamekuwa yaking’ang’aniwa na Karanja na Martha.
“Kesi hii haina uhusiano na kesi ya mauaji dhidi ya Karanja,” Jaji Mutuku alisema baada ya kuelezwa na kiongozi wa mashtaka Catherine Mwaniki “Karanja anasakwa kwa makosa yaliyotokea Gilgil. Kesi hiyo inashughulikiwa na Mahakama ya Naivasha.”
Jaji Mutuku alisema hawezi kushughulikia suala lilo katika mahakama tofauti.
Nje ya mahakama maafisa wanne wa polisi walimweleza Karanja , “ Sisi ni maafisa wa Polisi kutoka Gilgil tumeagizwa tukukumate kujibu shtaka la wizi wa mabavu.”
Karanja aliwasihi maafisa hao wa polisi wamruhusu awasiliane na mmoja wa familia yake kuchukua Jaketi “ kwa sababu Gilgil kuna baridi.”