ARI YA UFANISI: Anafaidi wakulima kupitia kituo cha kuwaelimisha mbinu tofauti
Na PETER CHANGTOEK
MVUA inayoendelea kunyesha na ambayo imepitiliza kiwango, katu haiwezi kumzuia Gachara Gikungu kuendelea kutoa mafunzo kwa hadhira yake kuhusiana na masuala ya kilimo, katika taasisi yake.
Tunakutana naye katika shamba la maonyesho lililoko umbali wa takriban kilomita tatu kutoka soko la Mia Moja, kwenye barabara kuu ya Meru-Nanyuki.
Shamba hilo la maonyesho, maarufu kwa jina Kilimo Biashara Resource Centre, lina wataalamu wa kilimo, ambao huwafunza wafanyakazi wa shambani pamoja na mameneja, ili kuwawezesha kuhakikisha kuwa mazao yanazalishwa kwa wingi shambani, huku rutuba mchangani ikidumishwa.
Gikungu, 60, ni mwasisi wa taasisi hiyo ambayo iko kwenye shamba la ekari nne, mnamo 2007, baada ya kustaafu mapema, na anaazimia kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo.
Gikungu huwahamasisha wakulima wasihangaike wakiyatafuta mashamba makubwa ya kuziendesha shughuli za zaraa, ilhali mashamba madogo pia yanaweza kuyazalisha mazao mengi yakitumiwa ipasavyo.
“Wakulima wanafaa kujiuliza kuhusu kinachohitajika ili kuukuza mmea fulani; kwa mfano viazi, na kupata ufahamu kuhusu yanayofaa kufanywa ili viazi vizalishe mazao mengi. Hili litawasaidia wakulima kujua kwamba hakuna haja kwao kulitumia shamba ekari moja, endapo yale yanayovunwa kwa ekari moja yanaweza kuvunwa kwa shamba robo ekari,’’ anasema,.
Anasema kuwa hoja si ukubwa wa shamba linalotumiwa, bali lililo muhimu ni mazao na jinsi ya kuitunza mimea shambani.
Katika taasisi hiyo ya mafunzo, wafanyakazi wa shambani na wakulima huhamasishwa kuzibadilisha nia zao, jinsi ya kuyatayarisha mashamba, jinsi ya kuchungua mchanga, uhifadhi wa maji mchangani, jinsi ya kulima shamba, na jinsi ya kukinga magonjwa na wadudu waharibifu shambani.
Aidha, hufunzwa jinsi ya kuyahifadhi mazao baada ya kuvunwa shambani, uzalishaji wa maziwa bora, uzalishaji wa mifugo, jinsi ya kuwatunza ndama, utengenezaji wa lishe ya mifugo, jinsi ya kuyateka na kuyahifadhi maji kwa kutumia teknolojia mpya, miongoni mwa mambo mengine mengi.
Anasema asilimia 90 ya wakulima ni watu wenye umri mkubwa, ilhali vijana wengi wapo mijini wakizitafuta ajira za afisini.
“Vijana wenye nguvu na elimu wamerundikana mijini wakitafuta ajira, au wakiwangoja wazazi wao wakongwe kuwalisha kwa sababu wanadhani kuwa ukulima ni wa waliostaafu au wale waliokosa mwelekeo maishani,’’ anasema mtaalamu huyo, ambaye pia ni mkulima.
Kubadilisha mbinu
Anaeleza kuwa endapo wakulima hawatabadilisha mbinu za uzalishaji na za kuyauza mazao yao, watasalia kuwa maskini, huku wengine wanaovuna wasikopanda, wakinufaika kwa kuwapunja kwa bei duni za mazao.
Zaraa, anasema mtaalamu huyo, hustawisha uchumi katika mataifa tofauti tofauti yaliyoko duniani.
“Kilimo huchukua nafasi kubwa sana katika ustawishaji wa uchumi wa nchi yoyote kwa kuwa huwapa wananchi chakula, ajira, riziki miongoni mwa manufaa mengine katika jamii. Na ili wakulima waendelee kujihusisha na shughuli zenye faida, ni lazima wadhihirishe kuwa wanawauzia wateja wao bidhaa zenye ubora wa kiwango cha juu, na kwa wingi,’’ anaeleza Gikungu.
Mtaalamu huyo anaongeza kuwa, wakulima ni sharti wahakikishe kuwa wana habari kuhusu mbinu zinazofaa ili kuzalisha mazao bora.