Bei za mafuta zapanda
Na CHARLES WASONGA
BEI ya mafuta iko juu petroli ikipanda kwa Sh2.54 kila lita, dizeli ikipanda kwa Sh2.65 nayo mafuta taa yakipanda kwa Sh2.98 jijini Nairobi; bei mpya za kuanza kutumika Ijumaa zimeonyesha.
Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Bidhaa za Petroli (EPRA) imesema sababu ya bei za juu kwa bidhaa hizi ni kutokana na kupanda kwa gharama za ununuzi mafuta ghafi yanayoingizwa nchini kutoka mataifa ya kigeni. Gharama hizo zimepanda kwa wastani wa asilimia 1.9 katika mwezi wa Oktoba.
Jijini Nairobi lita moja ya petroli aina ya super itakuwa ni Sh110.59 huku dizeli ikiuzwa Sh104.61 kila lita.
Lita moja ya mafuta taa kuuzwa Sh104.06 hadi Desemba 14, 2019, bei mpya zitakapotangazwa.
Bei hizo zinajumuisha ushuru wa thamani ya ziada (VAT) kulingana na hitaji la Sheria ya Fedha ya 2018 na viwango vipya vya ushuru wa uagizaji vilivyofanyiwa mabadiliko ili kuoana na viwango vya mfumkobei.
Oktoba 2019 EPRA ilipunguza bei za petroli na dizeli kwa kukata Sh4.76 na Sh1.08 kila lita mtawalia, lakini mafuta taa yakapandishwa bei kwa Sh0.44 kila lita ikilinganishwa na bei zilizokuwa zimetangulia.
Ina maana kwamba Oktoba petroli iliuzwa kwa Sh108.05 kwa lita, dizeli ikauzwa kwa Sh101.96 huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh101.08 jijini Nairobi.