Mechi za Gor Mahia kurejea Kisumu
Na CECIL ODONGO
UONGOZI wa klabu ya Gor Mahia yenye ufanisi mkubwa nchini Kenya umefutilia mbali marufuku ambapo mechi zake katika uga wa Moi, jijini Kisumu zilikuwa zimefutwa.
K’Ogalo iliweka marufuku hiyo kutokana na purukushani zilizotokea langoni mnamo Septemba, wakilaumu wahuni kwa kuteka nyara ukusanyaji wa ada za kutazama mechi na kuinyima klabu hiyo mapato.
Akizungumza na Taifa Leo, mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier alisema wamefutilia mbali uamuzi huo baada ya kuandaa mkutano wa kina na maafisa wa K’Ogalo kutoka Kisumu na kukubaliana kuhusu masuala yaliyoibua utata Septemba.
“Kwa sasa natangaza kwamba tumerejea Kisumu baada ya kusuluhisha masuala yaliyokuwa yakizua utata. Kisumu ndiyo ngome yetu na sasa nimefutilia mbali marufuku ya awali mara moja,” akasema Rachier.
Aidha, afisa huyo veterani alikiri kwamba klabu hiyo imekuwa ikijizolea mapato madogo kila inapocheza mechi zake katika viwanja vingine ikilinganishwa na Kisumu. Gor inatarajiwa kuchuana na Kakamega Homeboyz katika uga wa Moi kwenye mechi ya KPL.
“Mapato yetu yamepungua hasa wakati tunapoandaa mechi za katikati ya wiki. Kwa mfano tulikusanya tu Sh7,700 wakati tulipocheza dhidi ya Mathare United wikendi iliyopita. Tuna fursa nzuri ya kupata pesa tukicheza Kisumu kuliko Machakos,” akaongeza Rachier.
Vilevile Rachier alimtaka mwenyekiti wa Kakamega Homeboyz Cleophas Shimanyula akome kujigamba kwamba timu yake itashinda K’Ogalo, akisema baadhi ya matamshi ambayo amekuwa akitoa na kuchapishwa mitandaoni ni ya kukera na kichokozi.
“Siwezi kusema mengi kuhusu matamshi yake ila mimi najua matokeo ya mechi huamuliwa uwanjani. Watu walisema kwamba tungecharazwa na AFC Leopards lakini matokeo yalikuwa mengine na sasa wamenyamaza. Sisi tunasubiri soka isakatwe wala hatuna muda wa majibizano,” akasema Rachier.
Kujishasha
Shimanyula alikuwa amedai kwamba Kakamega Homeboyz itacharaza K’Ogalo hata wabadilishe uwanja wa kuandaa mechi hiyo ama washiriki mechi za kirafiki na timu kutoka nje akitaja hata Arsenal ya Uingereza.
Kurejeshwa kwa mechi hizo jijini Kisumu kunatarajiwa kuwafurahisha mashabiki wa Gor eneo hilo huku baadhi yao wakizama mitandaoni na kueleza furaha yao kuhusu uamuzi huo.
Gor wako nchini Misri ambao watasakata mechi ya kirafiki dhidi ya Al Ahli Tripoli mjini Alexandria hapo kesho.