Makala

MWANAMUME KAMILI: Heri upweke kuliko hadaa kama ilivyo katika ndoa za kidijitali

April 4th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

“Jamani mbona kuchukizana na kuhujumiana kama kwamba mmekwisha talikiana? Hivi ndivyo visa vinavyochukiza katika maisha ya wachumba na wapendanao. Mke anamwadhibu mumewe kwa kila njia. Mume vilevile. Heri upweke kuliko maisha hadaa kama ilivyo katika familia za leo”

Na DKT CHARLES OBENE

Kizazi cha leo hakithamini utu wala heshima. Si wanawake si wanaume. Hata wachumba wa leo wanatandikana makofi; wanapapurana, wanatibuana na kufokeana hadharani ilhali hawajawa wamoja!

Maharusi ndio kwanza mahasidi wanaolishana sumu! Vilivyotumainiwa kama vyumba vya mahaba vimegeuka nyanja za masumbwi kila uchao. Wanadamu si watu tena wanaoweza kushawishi wema.

Watajifunza nini kina yakhe ikiwa wangwana waliofunga ndoa za ajabu na waliofungua maisha katika fungate ndio kwanza wanaokwenda mahakamani kutamatisha mapenzi na kukoleza uadui?

Tufanyeje akina sisi tuliosubiri mwanga; tuliotumainia kunufaikia zenu akili ili nasi tujijenge na kukuza familia? Kama maharusi wa kanisani wanafumana mishale na kufedheheshana mahakamani seuze akina sisi tuliokutana kwenye mabaa tukapendana katika kumbi za densi?

Kila mara tunaposikia asili ya mizozo nyumbani tunasikitika na kufedheheka mno. La ajabu ni kwamba wanandoa au wachumba wa leo wanazozania vitu vya aibu mno. Si mavazi ya mke si chakula si simu si runinga si mashemeji si pesa si marafiki si wanaharamu.

Mbona wawili wasiweke mbele upendo kabla kuzozania mahitaji yao binafsi? Hili jambo la wanaharamu hunikeketa mno maini. Lau si ufidhuli na ujinga wa kitoto uliokita akilini mwa wanawake kwa wanaume wa leo, wachumba na wanandoa wasingalipigania malezi wa wanaharamu.

 

Kuchukia wanaharamu

Hakuna mtoto wa kitandani wala wa sakafuni.   Mwanamke au mwanamume kumbagua au kumchukia wanaharamu ndio msumari wa mwisho katika kaburi la mahaba. Hakuna mapenzi katika nyumba mlimojaa chuki na ubaguzi.

Waja kupatana hutegemea pakubwa uthabiti na ukomavu wa akili. Ndio maana wanawake kwa wanaume wa leo wanahimizwa kukomaa akili kabla kujitosa katika ukumbi wa mahaba.

Kufuata upepo wa mapenzi au kusukumwa na jazba za ujanani pasipo mtu kukomaa akili kumechangia pakubwa kuwepo wanandoa au wapendanao wanaochukiza kwa zao tabia za kitoto.

Nyumbani mlimojaa fujo na vita vya kila mara hakukaliki. Isitoshe, hakuwezi kukuza watoto katika maadili ya heshima, bidii na ukakamavu maishani. La ajabu ni kwamba baadhi ya familia za leo zipo katika njia hii panda.

Mke na mume hawasemezani kwa kuwa hakuna muamana baina yao.

Tuliweke wazi kwamba usununu na usumbufu wa baadhi ya wanandoa ndio mwanzo wa talaka. Uvumilivu unaweza vilevile kufika mfundani. Mwisho wa stahamala ni mambo kwenda segemnege!

 

Hakuna jazba

Haja gani kugeuka mahasidi wakati mmekwisha kuyavulia nguo na kukoga kwenye vidimbwi vyenu? Hakuna siri baina yenu. Hakuna jazba – watu kuwehuka – ambazo kuta hazijashuhudia. Isitoshe, kununiana siyo mwisho wa mahaba baina ya watu waliokwisha donana.

Jamani mbona kuchukizana na kuhujumiana kama kwamba mmekwisha talikiana? Hivi ndivyo visa vinavyochukiza katika maisha ya wachumba na wapendanao. Mke ana lazima kumwadhibu mume kwa kila njia.

Mume vilevile. Heri upweke kuliko maisha hadaa kama ilivyo katika familia za leo.

Kutofautiana baina ya mke na mumewe au baina ya wapendanao si tukizi maishani. Haya ni mambo yanayotokea kila mara na ambayo sharti tuyajulie kwa mapana. Hata hivyo, kuna vijimambo vya aibu vinavyochusha maisha ya wangwana binadamu wa leo.

Ubishani baina ya mke na mume ni sumu nyumbani. Si ajabu siku hizi kumwona mke akimwota mumewe dole puani na mume vilevile. Mwisho wa ugomvi huu ni mwanzo wa vita baridi vinavyoacha ukimya wa kaburi nyumbani.

 

Wakarimu nyumba ndogo!

Jamani wake kwa waume wa leo! Mtawezaje kununa nyumbani lakini mkawa wepesi wa ndimi tena wakarimu vilabuni au nyumba ndogo? Kama hasira,- basi na ziwe vivyo hivyo hata nje!

Angalau mjiepushe na kadhia zote kama kweli ni hasira! Mengineyo ni ujinga na utoto usiofaa muda kuujadili! Watu hawana budi kuwa watu wenye utu.

Vituko hivi tunavyoviona maishani ni ithibati ya jinsi binadamu walivyopungukiwa hekima na akili. Jukumu la watu wazima ni kutambua thamani ya uhusiano, hadhi ya familia na kujua vipi kusuluhisha vijimambo vya nyumba.

Wawili wanaopendana au wanaopendezana wanaweza kutofautiana wakazozana na mwishowe wakapatana na kuendeleza muamana pasipo haja kuvuana nguo hadharani au hata kufedheheshana mahakamani.

Maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga! Hivyo ndivyo afanyavyo mwanamume na mwanamke kamili.

 

[email protected]