• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Ronaldo aiweka Ureno pazuri Euro

Ronaldo aiweka Ureno pazuri Euro

Na MASHIRIKA

FARO, Ureno

CRISTIANO Ronaldo alidhihirisha weledi wake mbele ya goli alipopachika mabao matatu kwa mara yake ya tisa, huku Ureno ikizamisha Lithuania 6-0 Alhamisi, na kunusia tiketi ya kushiriki Kombe la Bara Ulaya (Euro) mwaka 2020.

Hata hivyo, mabingwa hao wa Bara Ulaya watasubiri hadi mechi ya mwisho kupigania tiketi ya kutetea taji lao, baada ya timu nambari tatu Serbia kunyamazisha wanyonge Luxembourg 3-2, katika mechi nyingine ya Kundi B.

Ronaldo hakuwa amechezeshwa dakika zote 90 na kocha wa Juventus Maurizio Sarri katika mechi mbili zilizopita, huku Mwitaliano huyo akidai kuwa mshambuliaji huyo anasumbuliwa na jeraha la goti.

Ripoti zinasema kuwa aliondoka uwanjani kabla ya mechi kutamatika alipoondolewa na Sarri kwenye mchuano wa Ligi Kuu ya Italia dhidi ya AC Milan, ambao Juve ilishinda 1-0 wikiendi iliyopita.

“Nilijua Ronaldo anaweza kucheza,” alisema kocha wa timu ya Ureno Fernando Santos baada ya mechi.

“Mchuano huu unaondoa wasiwasi kuhusu hali yake ya kimwili, kwa wale waliodhani hayuko fiti. Mimi binafsi sikuwa na tashwishi, na nilisema hivyo.”

Ureno inashikilia nafasi ya pili kwa alama 14. Ukraine, ambayo tayari imefuzu, inaongoza kwa alama 19.

Ureno iko alama moja mbele ya Serbia. Wareno watanyaka tiketi ya Euro 2020 wakilemea Luxembourg hapo kesho. Serbia pia itasakata mechi yake ya mwisho hiyo kesho dhidi ya Ukraine.

Ronaldo sasa amefungia Ureno mabao 98 katika mechi 163, na atatumai kuwa mchezaji wa pili katika historia ya soka kufungia timu yake ya taifa mabao 100.

Raia wa Iran, Ali Daei ndiye anayeshikilia rekodi hiyo, baada ya kufungia taifa lake mabao 109 katika mechi 149, kati ya mwaka 1993 na 2006.

Ronaldo alifungua ukurasa wa mabao kupitia penalti kunako dakika ya saba alipooangushwa ndani ya kisanduku, kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 22.

Pizzi afunga bao la tatu

Kiungo wa Benfica, Pizzi alifuma wavuni bao la tatu dakika ya 52 kabla ya Goncalo Paciencia na Bernardo Silva kuimarisha idadi hiyo hadi magoli 5-0 walipocheka na wavu dakika za 56 na 63 mtawalia. Ronaldo alihitimisha “Hat-trick” yake dakika ya 65. Sasa amefunga mabao matatu katika mechi moja kwa mara yake ya 55 tangu aanze kusakata kabumbu.

Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 34 amefungia Ureno mabao 13 katika mechi saba zilizopita.

Alikosa fursa ya kufikisha mabao 99 baada ya kupiga nje shuti kutoka yadi 10.

“Hat-trick” zingine za Ronaldo ni 44 akiwa Real Madrid, moja akiwa Juventus na nyingine akichezea Manchester United.

You can share this post!

TAHARIRI: Ufisadi huu utaua spoti yetu kabisa

Majeraha kikosini Harambee Stars iliyoshtua Misri

adminleo