MAKALA MAALUM: Idara ya polisi haijapiga hatua kubwa katika kuleta mageuzi
Na STELLA CHERONO
SWALI la iwapo mageuzi ambayo yamekuwa yakitekelezwa katika idara ya polisi yamefanikiwa au la bado ni kitendawili, iwapo matukio yanayoendelea kuzingira maafisa hao wa usalama nchini ni ya kuzingatiwa.
Aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Joseph Boinnet ambaye kwa sasa ni Waziri Msaidizi, alipigia debe mageuzi hayo wakati akiondoka ofisini baada ya kukamilisha muda wake wa kuhudumu kulingana na Katiba.
Bw Boinnet alisema idara hiyo ilishuhudia mageuzi makubwa chini ya uongozi wake. Alitaja kuunganisha kwa idara za polisi wa kawaida na wale wa utawala kama mojawapo ya ufanisi alioafikia, akisema hilo lilisaidia kufanikisha utoaji wa huduma bora na kuhakikisha kwamba majukumu ya vitengo hivyo viwili havigongani.
Mtaala
Mafanikio mengine aliyoyataja ni kubadilishwa kwa mtaala wa mafunzo kwa makurutu wanaoajiriwa kama polisi, kuimarika kwa mbinu ya kuhakikisha kwamba maslahi ya maafisa yanaangaliwa, makazi bora na kupewa huduma za bima ya matibabu kwa polisi binafsi pamoja na familia zao wanapougua.
“Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) imepitia mageuzi makubwa kutoka kwa miundombinu bora hadi mishahara ya polisi, vifaa, mavazi na kujihami kwa maafisa kupambana na utovu wa usalama unaochipuka mara kwa mara nchini,” akasema Boinnet alipokuwa akitoa hotuba hiyo ya mwisho.
Msingi wa kauli ya Boinnet ulitokana na sheria iliyopitishwa mwaka 2011, ambayo ilitoa mwongozo jinsi ambavyo idara hiyo inaweza kuasi dhana ya kutumia mamlaka kuadhibu raia bila makosa, na badala yake polisi kufanya kazi yao kulingana na kanuni za taaluma yao.
Hata hivyo, miaka minane baada ya mchakato wa mageuzi hayo kung’oa nanga, polisi wengi bado wanahangaika na kupitia changamoto tu kama zamani, licha ya serikali kutumia zaidi ya Sh10.3 milioni kwenye bajeti ya mwaka 2015-2018 kuwajengea makazi mapya.
Ni kutokana na hayo ambapo mashirika ya kijamii, wachanganuzi wa masuala ya usalama na watetezi wa haki za kibinadamu wanaamini kwamba, mageuzi katika idara ya polisi yamefeli pakubwa licha ya serikali kuwekeza mabilioni ya fedha kubadilisha kitengo hicho muhimu cha usalama.
Kulingana na mwenyekiti wa kundi ambalo limekuwa likifuatilia mageuzi hayo PRWG-K, Bw Peter Kiama, hakuna hatua kubwa zilizopigwa katika mageuzi yaliyolengwa, kutokana na uhasama na ubinafsi wa wakuu wa polisi. Hii ni licha ya baraza la mawaziri mnamo 2009 kupitisha ripoti ya Ransley iliyotoa mwongozo wa kufanikisha mageuzi katika idara hiyo.
“Kuna tabia za uhalifu zinazoendelezwa katika idara ya polisi. Uchunguzi, mohajiano na ukaguzi wa maafisa wa polisi ambao ulipangwa kutekelezwa ili kusafisha idara hiyo, ulikosa kuzaa matunda. Asasi ambazo zinaangazia utendakazi wa polisi zimekuwa zikisimamiwa na watu wanaoongozwa na maslahi yao ya kibinafsi, na kusahau kutekeleza majukumu yatakayosaidia kuboresha idara hiyo,” akasema Bw Kiama.
Katika muda wa miezi michache iliyopita, Wakenya wameshuhudia kukamatwa kwa maafisa wa polisi ambao walihusika katika visa vya wizi wa fedha katika benki, hoteli na barabarani. Wengine nao walipatikana na pembe za ndovu, miongoni mwa maovu mengine.
Tume kama Mamlaka ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi (Ipoa), Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC) na asasi ya Huduma kwa Polisi (NPS), zote zimefeli kutekeleza wajibu wao. Utepetevu huo umekashifiwa mno na mashirika ya umma pamoja na yale ya kutetea haki za kibinadamu chini ya mwavuli wa PRWG-K, ambazo zimelaumu idara ya polisi kwa ubadhirifu wa pesa za mlipa ushuru bila kutimiza malengo yoyote.
Jeruhi mwanafunzi
Kudhihirisha namna idara ya polisi bado ni ile ile, maafisa watano wa usalama Jumatatu wiki hii waliwapiga na kuwajeruhi vibaya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), waliokuwa wakishiriki maandamano chuoni humo.
Watano hao walinaswa kwenye video wakiwaangushia wanafunzi hao kipigo kikali, na kumfanya Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i pamoja na Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) wa sasa Bw Hillary Mutyambai kushutumu kitendo hicho. Vile vile, waliwasimamisha kazi polisi hao ambao walikuwa wameshutumiwa vikali kwenye mitandao ya kijamii kwa ukatili wao.
Kupitia taarifa, Dkt Matiang’i alieleza kughadhabishwa na jinsi maafisa hao walikabili wanafunzi ambao walikuwa tu wakilalamikia ukosefu wa usalama ndani na nje ya chuo hicho.
“Nimefuatilia matukio katika chuo cha JKUAT na nimeshangazwa na mkondo wa mambo. Polisi walitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wanafunzi hao kinyume na amri ya idara,” akasema Dkt Matiang’i.
IPOA nayo ilishutumu kisa hicho na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya maafisa waliohusika.
“IPOA inakemea vikali tukio la JKUAT ambapo polisi walinaswa kwenye kamera wakiwapiga wanafunzi bila huruma,” ilisema sehemu ya taarifa iliyotiwa saini na mwenyekiti wa IPOA Anne Makori.
Hata hivyo, IPOA imekuwa na vita vya ndani kwa ndani vilivyosababisha kutimuliwa kwa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji Maina Njoroge, miezi mitano tu baada ya kuchukua wadhifa huo kutoka kwa Joel Mabonga ambaye alistaafu mwaka jana.
Utendakazi
Ni kutokana na vita hivyo ambapo maafisa wa PRWG-K wameeleza wasiwasi wao kwamba, utendakazi huru wa mamlaka hiyo unavurugwa na maafisa wanaochimbiana na kuendeleza uhasama kati yao.
“Bodi ya IPOA haiwajibiki ipasavyo. Wameangazia sana nyongeza ya mishahara, ulinzi na masuala mengine ambayo yanawahusu binafsi,” alieleza Bw Kiama.
Anaongeza kwamba, mahojiano na uchunguzi wa polisi ambao unalenga kuleta uwajibikaji katika idara hiyo, ni kati ya mambo yaliyofeli kabisa.
Ni wiki jana tu ambapo maafisa wa polisi waliokuwa na kesi baada ya kuhojiwa na NPSC, walirejeshewa kazi zao licha ya Sh800 milioni kutumika kuwachunguza na kuwasimamisha kazi.
NPSC pia ilitangaza kwamba maafisa hao hawatachukuliwa hatua zozote za kinidhamu kutokana na uchunguzi huo uliofanywa kabla yao kuingia ofisini.
Mwenyekiti mpya wa NPSC Eliud Kinuthia alisema tume hiyo imeamua kutupilia mbali mapendekezo ya mtangulizi wake Johnstone Kavuludi dhidi ya maafisa hao, na kwamba kuhojiwa na kuchunguzwa kwa maafisa wa vyeo mbalimbali umesimamishwa mara moja.
“Tutawapa nafasi nyingine ya kujitetea. Kulingana na maafisa wapya wa tume, mapendekezo yaliyotolewa baada ya kuhojiwa na kuchunguzwa kwao hayana mashiko na yametupiliwa mbali,” akasema Bw Kinuthia.
Mageuzi katika idara ya polisi, ambayo yana nia ya kutumia teknolojia katika idara hiyo, yametumia zaidi ya Sh450 bilioni kuwekeza miundomsingi ya kisasa kwenye idara hiyo.
Miundombinu hiyo ni katika sekta ya mawasiliano ya kisasa, magari ya polisi, vituo vya kuongoza operesheni, helikopta mpya kati ya mingine.
Mashirika ya umma na yale ya haki za binadamu kupitia mwavuli wao wa PRWG-K, sasa yanapendekeza kutekelezwa kwa kifungu cha sheria ya Polisi kinachompa Inspekta Jenerali mamlaka ya kusimamia bajeti ya maafisa wake, ili kuhakikisha kila kituo cha polisi na vitengo vyote viko na fedha za kutosha kuendesha shughuli zao.