• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Changamoto ya kuwa mcheshi ungali chuoni

Changamoto ya kuwa mcheshi ungali chuoni

NA STEVE MOKAYA

EZRA Kerosi ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Baraton. Alisomea katika shule ya upili ya Mang’u, na kuhitimi mwaka wa 2017.

Mbali na kusomea uhandisi, anatumia muda wake mwingi katika kukuza talanta yake ya ucheshi, maana anaamini kuwa ndiyo itamsaidia sana maishani, kuliko masomo.

“Ulifika wakati nikaona kuwa uhandisi unahitaji kujitolea sana na unachukua muda mwingi, hivyo nikapanga kuacha masomo na kufuata ndoto yangu ya kuwa mcheshi,” Ezra anasema.

“Ila tulipozungumza na wazazi nyumbani, nikaona nizidi kusoma huku nikikuza talanta,” anongeza.

Bw Kerosi, mwenye umri wa miaka kumi na tisa, anasema kuwa mwanzo wake katika sanaa ya ucheshi umekumbwa na mseto wa changamoto na mafanikio sawia.

Anasema kuwa baadhi ya wanafunzi na walimu katika darasa lake humwona kama mtu asiye makini masomoni.

Hata jamaa wake walijaribu kumshawishi aache suala zima la ucheshi na atie bidii masomoni, ila walipogundua kuwa ana ari kubwa, wakaanza kumtia moyo na kumsaidia kwa njia mbalimbali.

“Mwanzo walisema kuwa nitawaletea aibu kwa kufanya ucheshi, lakini sasa wamenielewa vizuri. Saa hii wazazi wangu hunipa pesa za kuenda katika majaribio ya ucheshi, pamoja na za kupanga baadhi ya tamasha humu chuoni.”

Anasema kuwa ameenda katika majaribio mbalimbali ya ucheshi, yakiwemo yale ya Churchill Live, ila akaambiwa atie bidii katika mambo kadhaa. Kwingine wanamwambia angoje majibu, ila hadi sasa bado majibu hayajaja.

Licha ya hayo, Kerosi anazidi kuwekeza, akili, muda na hata pesa katika penzi lake. Amewahi kuandaa tamasha ya ucheshi chuoni mwao, na anasema kuwa watu walijaza ukumbi wote.

Ni katika tamasha hiyo alipowatambua wanafunzi wenza wenye talanta za kuigiza na kuchekesha, na jambo hilo lilichochea moto wake uliokuwa umeanza kufifia.

Hata hivyo, anasema kuwa moja ya changamoto kuu anazopitia zinatokana na usimamizi wa chuo. Anasema kuwa inakuwa vigumu kupewa kibali cha kuandaa tamasha katika ukumbi wa chuo. Kadhalika, anaongeza kuwa shughuli nzima ya kufanikisha tamsha hizo huwa kazi pevu kwake.

“Nimewahi kulia mara kadhaa. Hebu fikiria hata wewe- mimi ndiye napanga kila kitu, nasimamia shughuli nzima na kuwaandaa watu watakaoburudisha umati. Mtu huchoka, na kama huna moyo utaacha.”

Kerosi huigiza vipindi vyake pamoja na wanafunzi wenza chuoni humo, wenye nia sawia, na wakati mwingine peke yake.

Anachapisha kazi zake katika mitandao ya kijamii kama vile Youtube, Facebook na Instagram. Hata hivyo, anasema kuwa wakati mmoja alikufa moyo katika safari hii na hata akavifuta vipindi vyake vyote kutoka kwenye mitandao hiyo. Ila akajirudi tena halafu na kuvichapisha tena.

Ili kuhakikisha kuwa anafanya kazi ya darasani barabara na pia kuimarisha kipaji chake, Kerosi anasema hivi:

“Huwa ninarauka ili kufanya mazoezi na kudurusu vichekesho vyangu. Pia huwa nafanya vivyo hivyo usiku baada ya kufanya kila kitu, kabla nilale.”

Anasema kuwa analo daftari maalumu la kuandika mawazo ya vichekesho. Anatembea na daftari hilo popote aendapo. Anasemna kuwa anaandika wazo lolote la kuchekesha linapomjia, mahali popote.

Kerosi anamtazamia Rawan Atkinson, almaarufu kama Mr Bean ama Johnny English. Anasema kuwa anafuata nyayo zake sana kwa sababu yeye ni miongoni mwa wachekeshaji hodari sana ulimwenguni, ambao pia ni wasomi. Johnny Englisha alifanya Uzamifu katika uandisi kutoka kwenye chuo kikuu cha Oxford.

Ezra Kerosi anapanga kuwekeza sana katika biashara ya uchekeshaji, ili akuze vipaji, na pia atimize ndoto yake. Anasema kuwa uhandisi anausomea tu ili kujifurahisha, maana hatazamii kufanya uandisi sana baadaye.

Kadhalika, anawashukuru wale wanafunzi wenza ambao humtia moyo wakati wengine wanamkashifu. Anamshukuru Daktari Mooka, ambye ni mhadhiri katika chuo kikuu cha Baraton, kwa kumtia moyo na kumpa wosia.

You can share this post!

Boma la Rais lapasuka zaidi

Mwanafunzi amtandika mwalimu katika fumanizi la uroda...

adminleo