OBARA: #KOT hawajaiva kuchochea mageuzi ya kweli nchini
Na VALENTINE OBARA
WIKI iliyopita, mtandao wa kijamii wa Twitter ulisheheni jumbe za Wakenya walioonekana kuwa na hasira kwa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.
Hii haikuwa mara ya kwanza Wakenya wanaotumia Twitter, almaarufu kama #KOT kujumuika kwa njia hii dhidi ya serikali.
Wao hufanya hivyo kila wanapochukizwa na jambo lolote lile na kuna wakati wanafanikiwa kupata wanachotaka hasa inapohusu maswala ya haki za kijamii.
Wakati huu, baadhi ya #KOT walimtaka Rais ajiuzulu baada ya kunukuliwa akishangaa kwa nini Wakenya wanaumia kiuchumi, huku wengine wakitaka avunje baraza lake la mawaziri.
Kila mara hali kama hii inaposhuhudiwa mitandaoni, baadhi ya wananchi na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu hutumai hatimaye Wakenya wamezinduka na wanajitokeza kimasomaso kupigania uongozi bora.
Lakini ‘hasira’ hizo huwa hazidumu muda mrefu wala kukaribia kugeuka maandamano barabarani.
Hii ni ishara kwamba mapinduzi au mageuzi makuu ya utawala wa nchi hayataanzishwa hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii jinsi imefanyika katika mataifa mengine.
Kando na kuwa #KOT wana desturi ya kupata jambo jipya la kuchangamkia kila baada ya saa chache na kuwafanya kusahau lile la awali, mitandao kama vile Twitter imejaa watumizi ninaoweza kuwataja kuwa wawekezaji.
Wawekezaji hao ambao wana maelfu ya wafuasi hulipwa na watu binafsi, mashirika au vyama kuvumisha bidhaa, huduma au hoja. Vilevile, wengine hulipwa kufifisha hoja inayovuma kwa kuanzisha hoja tofauti.
Wanaaminika kuwa na ushawishi mitandaoni kwa msingi wa ufuasi walio nao. Wana uwezo wa kufanya hoja ivume kwa kuvutia watu wengi kuijadili.
Kutokana na kuwa wanalipwa, hoja hizi hazidumu kwa muda mrefu na pia si rahisi kuaminika kuwa za uaminifu. Kwa hivyo si rahisi kujua kama kweli wananchi huwa wamechoshwa na utawala uliopo, au wanafanya hivyo tu kwa vile ni hoja iliyovumishwa na wawekezaji mitandaoni.
Kuchochea mageuzi ya kuleta uongozi bora kupitia mitandao ya kijamii itafanikiwa ikiwa tu #KOT watakuwa na nia hiyo kutoka moyoni mwao au kama anayegharamia hoja aina hizo amejitolea kwa maslahi ya umma bali si kwa nia ya kuchafua jina la utawala uliopo kwa manufaa yake ya muda.