• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Wakazi wa Ruiru waandama wakilalama kuhusu barabara mbovu

Wakazi wa Ruiru waandama wakilalama kuhusu barabara mbovu

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa mtaa wa Kwa Kairu mjini Ruiru, waliandamana Ijumaa wiki jana kwa sababu ya ubovu wa barabara za eneo hilo.

Walisema serikali ya Kaunti ya Kiambu tayari imewasahau ambapo wameachwa bila wa kuwajali.

Mfanyabiashara wa eneo hilo Bw Gitau Mugo alisema watakuwa wakiendesha maandamano hayo kila Jumatatu ili viongozi waliochaguliwa wazinduke popote walipo.

“Biashara nyingi katika sehemu hii zimefifia kwa sababu barabara ni mbovu zikiwa na mashimo mengi kila mahali. Kunaponyesha, masaibu yetu huongezeka maradufu,” alisema Bw Mugo.

Alisema tayari wanapanga kuchanga fedha ili kutafuta mbinu ya kujitengenezea barabara hiyo.

“Ama kwa kweli hatutaki kuingiza siasa kwa jambo hili lakini viongozi wa eneo hili wajue tunapitia hali ngumu,” alisema Bw Mugo.

Mfanyabiashara mwingine, Bw Benard Kiragu, alisema tangu wachague viongozi mwaka wa 2017, hakuna yeyote amerejea mashinani kujionea maendeleo.

“Kutoka mwaka ujao sisi kama wakazi wa hapa hatutalipia ushuru kwa kaunti ya Kiambu. Tayari inaelewa vyema ya kwamba haijatufanyia lolote la kujivunia,” alisema Bw Kiragu.

Naye mkazi wa eneo hilo, Bi Nancy Kariuki alisema siku hizi watu wengi wamesusia kuabiri pikipiki za bodaboda kwa sababu barabara ni mbovu kabisa.

“Wiki moja iliyopita mwanamke mmoja mjamzito aliangushwa chini na pikpiki ya bodaboda ambapo, hata la kusikitisha zaidi ilibidi kujifungua mtoto kando ya barabara,” alisema Bi Kariuki.

Akaongeza: “Tayari  ni wazi kuwa serikali ya Kaunti ya Kiambu imetuacha tujitegemee kivyetu bila kujali masilahi yetu,” Sisi tunataka kutendewa haki ili nasi tuweze kuwa kama wakazi wengine.”

Bw John Ng’ang’a ambaye ni mwenyekiti wa wahudumu wa bodaboda eneo la Kwa-Kairu, mjini Ruiru, alisema wanachama wake tayari wamepoteza biashara kwa sababu wateja siku hizi wanatembea miguu badala ya kubebwa kwa pikipiki.

“Wahudumu wa bodaboda wengi wenye mikopo wamelazimishwa kurejesha pikipiki madukani walikozinunua kwa sababu hawawezi kulipia madeni yao kwa wakati,” alisema Bw Ng’ang’a.

Bw Mung’ara Wanjoki ambaye ni mkazi wa Ruiru, alisema wakazi wa eneo hilo wamedangany’wa vya kutosha na kwa hivyo “viongozi wajitokeze wazi watuambie wanataka nini na wananchi.”

“Jambo linalotukera kabisa ni ukosefu wa usalama na kupewa kituo cha polisi. Alisema ifikapo saa mbili za usiku wahuni husumbua wakazi wa hapa kwa kuwapora mali yao. Kwa hivyo, walinda usala wanastahili kupiga doria kila mara,” alisema Bw Wanjoki.

Alisema majumba makubwa ya kibiashara yamekuwa mahame kwa sababu ya ubovu wa barabara hiyo huku akitoa mwito viongozi husika wafanye jambo la dharura.

You can share this post!

SIHA NA LISHE: Huzioka keki kwa kutumia unga asilia

Bandari, Storms watia fora vikapuni

adminleo