Habari Mseto

Arati na Didmus Barasa wazika tofauti zao

November 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Kimilili Didmus Barasa na mwenzake wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati wamezika tofauti zao wiki mbili baada ya kukamilika kwa uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra.

Itakumbukwa mnamo Novemba 7, 2019, siku ya upigaji kura Bw Barasa alizabwa makofi na kundi la watu mbele ya Bw Arati ambaye alionekana kuwatia shime.

Video iliyosambaa mitandaoni, Bw Barasa anaonekana akisalimiana na Bw Arati katika kituo cha upigaji kura cha uwanja wa DC.

Lakini Bw Arati anasikika akimjibu kwa maneno makali kwa kumwambia hivi: “Usiongee mbaya, unataka ukimbizwe saa hizi?. Leo mtakimbizwa. I can decide (ninaweza nikaamua) mkimbizwe saa hizi!”

Lakini Bw Barasa aliyeonekana kuingiwa na woga akamjibu; “Sisi ni friends, we are colleagues.” (Sisi ni marafiki, wewe ni mwenzangu).

Ghalfa bin vu! Bw Barasa alisukumwa na kundi la vijana ambao walinyakua kofia yake na kuanza kumchapa makofi kadhaa.

Kisa hicho kilishutumiwa vikali na watumiaji mitandao ya kijamii huku wengine wakipendekeza kuwa Bw Arati akamatwe na polisi na ashtakiwe.

Ajitetea

Hata hivyo Bw Arati alijijitetea akisema kuwa hakufanya kosa lolote na kwamba asingeingilia kati Bw Barasa angeumia zaidi.

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa alidai kuwa kundi la vijana waliokodiwa na Bw Arati walimjeruhi Bw Barasa na kumdunga sindano yenye sumu. “Mheshimiwa Barasa sasa amelazwa katika Hospitali moja nchini Afrika Kusini baada ya kudungwa na sumu huku Kibra. Ama kwa hakika ODM ni kundi la kigaidi wala sio chama cha kisiasa,” akasema wiki jana.

Lakini Jumanne wawili hao wameonekana wakitembea pamoja katika ndani ya majengo ya bunge huku wakionekana wenye furaha.

“Hayo ya Kibra yaliisha. Tunaendelea na maisha na urafiki wetu kama kawaida. Siasa ni kama mechi ya soka. Baada ya mechi kutamatika walioshindwa na walioshinda hukumbatiana na kuendelea na maisha kama kawaida,” Bw Barasa akawaambia wanahabari.

Na Bw Arati akasema: “Kazi yetu Kibra iliishi. Sasa sina shida na Didmus. Tuko pamoja na hata tumeshiriki chakula cha mchana pamoja.”