• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
Shule binafsi zafanya vyema katika KCPE 2019

Shule binafsi zafanya vyema katika KCPE 2019

Na LAWRENCE ONGARO

SHANGWE na vigelegele vilitanda katika Shule ya Msingi ya St Luke’s ACK, Thika Magharibi baada ya Joan Wanjiru, kutangazwa kuwa wa kwanza akiwa amejizolea alama 429 katika matokeo ya KCPE 2019.

Walimu na wazazi walifurika katika shule hiyo ili kushangilia ushindi wa mwanafunzi huyo ambaye aliandamana na mamake mzazi Bi Emma Wangari.

Wakati wa mahojiano na Taifa Leo mwanafunzi huyo alisema kilichofanya afikie kiwango hicho ni kutia bidii masomoni, kuwa na mwelekeo mmoja kwa maana ya kukijua cha kulenga pamoja na kudumisha nidhamu.

“Ama kwa kweli nilikuwa nikijisomea mwenyewe nilipokuwa peke yangu nyumbani huku wazazi wangu pia wakinitia shime nifanye bidii,” alisema Wanjiru.

Alisema tamanio lake kubwa ni kujiunga na shule ya kitaifa ya Moi Girls Eldoret huku akikamia kusomea udaktari wa kuzingatia akili atakapokamilisha elimu ya sekondari.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw Simon Gitonga, alisema wanafurahi sana kwa kupata sifa ya kipekee kutoka kwa mwanafunzi huyo ambaye wakati wote alikuwa na nidhamu na mtiifu kwa jambo lolote alilofanya.

“Kwa wazazi ambao watoto wao pengine hawakufanya vyema, ningetaka kuwashauri wasikate tamaa kwani bado watoto hao wana talanta tofauti kando na masomo. Kwa hivyo, wajaribu kukuza vipaji hivyo,” akasema Bw Gitonga.

Alitoa mwito kwamba wanafunzi waliofanya vyema wapewe nafasi ya kujiunga na shule za kitaifa walizochagua.

Mchungaji mkuu wa kanisa la ACK St Luke’s Thika Bw Solomon Thiga alisema maombi yao ilikuwa gunzo kwa ufanisi wao.

Tunafurahi kwa kupiga hatua hiyo na tunatarajia wanafunzi wetu wengi watajiunga na shule za upili,” alisema Bw Thiga.

Katika shule ya Glory Academy ya kanisa la AIPCA Thika Mwanafunzi Salem Nyoike Njoroge alikuwa wa kwanza baada ya kujizolea alama 423.

Mwanafunzi wa Glory Academy AIPCA Thika, Salem Nyoike Njoroge akiwa na wazazi wake. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema bidii yake ilitoa mchango mkubwa kwake yeye kuzoa alama hizo.

“Matarajio yangu ni kujiunga na shule ya upili ya Mang’u na lengo langu kuu ni kuwa Mhandisi,” alisema mwanafunzi huyo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw James Waicha alisema ushirikiano mzuri baina ya wanafunzi, walimu pamoja na wazazi umeleta matokeo hayo mazuri.

“Tunatarajia wanafunzi wapatao 14 kujiunga na shule za upili za kitaifa. Tunashukuru wazazi kwa kutuunga mkono kila mara tulipokuwa na wanafunzi hao,” alisema Bw Waicha.

Bw John Njoroge Nyoike ambaye ndiye babake mwanafunzi huyo, alisema huyo ndiye mtoto wake wa kwanza – kifungua mimba – na anatarajia atafanya vyema katika masomo ya shule ya upili.

Alisema mtoto wake ni mtu mwenye heshima na nidhamu na ndiyo maana alijizatiti na kufanya vyema.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sheng haina mashiko wala miaka...

Unai ndiye asili ya masaibu Arsenal – Nyota

adminleo