Rahma Education Centre ya Eastleigh yawika KCPE 2019
Na WANDERI KAMAU
SHULE ya Msingi ya mmiliki binafsi ya Rahma iliyo katika mtaa wa Eastleigh, Kaunti ya Nairobi ni miongoni mwa zile zilizoandikisha matokeo bora ya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) 2019.
Ingawa ilianzishwa miaka kadhaa iliyopita, Zubeir Abubakar aliibuka bora kwa kuzoa alama 393.
Hii ni ikilinganishwa na mwaka 2018, ambapo mwanafunzi bora alizoa alama 367.
Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa shule hiyo Bi Fatma Mutiso, juhudi hizo zimetokana na ushirikiano mzuri kati ya wanafunzi na walimu.
“Tungali shule changa kwani huu ni mwaka wa nne kwa watahiniwa kwa Darasa la Nane kufanya mtihani wa KCPE. Tunatarajia kwamba matokeo yetu yataendelea kuwa bora zaidi,” akasema Bi Mutiso kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’
Bi Mutiso alisema kuwa wanaimarisha mikakati kuhakikisha kuwa wamefanikiwa zaidi katika miaka ijayo ili kuhakikisha kuwa wanafunzi zaidi wanapata alama za kuwawezesha kujiunga na shue za kitaifa.
“Tunaamini kuwa wanafunzi wengi nchini wana uwezo mkubwa kimasomo lakini tatizo kuu limekuwa kupata mazingira bora kudhihirisha uwezo wao. Hata hivyo, juhudi zetu zitakuwa kuhakikisha kuwa tunawashirikisha wadau wote ili kuwawezesha kutoa mchango unaofaa kwa manufaa ya shule yetu,” akasema Bi Mutiso.
Kwa upande wake, Barobaro Abubakar alisema kuwa angependa kuwa mhandisi atakapojiunga na chuo kikuu. Alisema kuwa analenga kujiunga na Shule ya Upili ya Lenana.
Aliwashukuru walimu na wanafunzi wenzake kwa kubuni mazingira bora ya kimasomo ambayo yalimwezesha kupata matokeo hayo.