Habari Mseto

RIZIKI: Utengenezaji sharubati ni kazi anayofurahia kukidhi kiu ya wateja

November 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

MATAMANIO ya kila kijana ni kupata ajira ya ofisi na yenye mshahara mzuri hasa awapo amekamilisha elimu ya chuo kikuu au taasisi ya elimu ya juu.

Hilo kwa wengi hata hivyo linaendelea kuwa gumu kwa sababu ya uhaba wa kazi za aina hiyo nchini. Badala yake, kampuni, viwanda na mashirika, yanachuja wafanyakazi, kampuni zingine zikiishia kufungwa kwa wanachotaja kama kushindwa kuendesha gange zake kwa sababu ya uchumi kuzorota.

Hatua hiyo inafisha moyo miongoni mwa vijana, ikikumbukwa kuwa kila mwaka maelfu wanafuzu kwa vyeti vya kozi tofauti kutoka taasisi mbalimbali za elimu. Ni wazi nafasi za ajira Kenya ni finyu, kutokana na hali inayoshuhudiwa.

Baada ya kuhitimu kwa Stashahada ya Masuala ya Biashara (BA) miaka kadhaa iliyopita, Ann Wambui alitafuta kazi miaka miwili mfululizo bila mafanikio. Aliamua kuingilia biashara ili kutega riziki na kusukuma gudumu la maisha.

Alifanya biashara aina mbalimbali ikiwamo uchuuzaji wa nguo. Mnamo 2017, Wambui aliwekeza katika uwekezaji wa utengenezaji wa sharubati.

Huunda sharubatihai kwa matunda, miwa, Aloe vera (mmea asilia unaoaminika kuwa dawa ya kutibu maradhi ainati), viazisukari (beetroots), tumeric na tangawizi, miongoni mwa mimea mingineyo.

“Juisi ninayotengeneza haina kemikali yoyote na ina manufaa anuwai kiafya,” anaeleza mwanadada Wambui.

Isitoshe, ina ladha tamu na rangihai itokanayo na bitiruti na matunda ya kijani kama vile ndimu na matundadamu (tree tomato).

Kulingana na mjasirimali huyo, ilimgharimu mtaji usiozidi Sh20,000.

Alinunua chombo maalum kusaga matunda na kuyachanganya na mimea mingine kijulikanacho kama blender, ikiwa ni pamoja na pesa za kukodi chumba.

“Pia nilitafuta leseni kutoka kwa halmashauri ya jiji na idara ya afya,” Wambui akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano katika duka lake kutengeneza sharubatihai eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Hata ingawa utangulizi haukuwa rahisi, anasema kazi hiyo imeimarika kiasi cha kumudu kununua mashine ya kumenya miwa itoe juisi, iliyogharimu kiasi cha Sh60,000. Miwa inasifiwa kuwa na sukari halisia, ambayo haijachakatwa.

Sukari ya miwa ni nzuri kwa mwili kwani ina virutubisho na madini anuwai. Wataalamu wa masuala ya afya wanasema sharubati yake ina uwezo kuupa mwili nguvu kwa sababu ya glucose iliyopo.

Bi Ann Wambui, mtengenezaji wa sharubati ambapo hutengeneza juisi, kwa malighafi kama vile miwa, matunda, aloe vera, bitiruti, tumeric na tangawizi, miongoni mwa mimea mingine asilia. Picha/ Sammy Waweru

Miwa imesheheni Vitamini na madini kama Chuma, Potassium, Phosphorus na Calcium. Hali kadhalika, zao hilo linaorodheshwa katika jamii ya mimea yenye alkali, yenye uwezo kupambana na Saratani ya kibofu cha mkojo na matiti.

Juisi ya miwa ikichanganywa na matunda, mimea asilia kama aloe vera, bitiruti, tumeric, karoti, na tangawizi, na mingineyo, Ann Wambui anasema ina umuhimu mkubwa kiafya kwa mnyaji, hivyo basi wateja hufurika. “Hupika kwa glesi, ile ndogo ni Sh30 ilhali kubwa Sh50,” adokeza.

Pia, ana huduma za kupakia wateja wanaochukua bidhaa na kuondoka moja kwa moja zikatumike kwingineko kama vile wenye wagonjwa hospitalini au wale wa kupelekea wana wao.

“Aghalabu kwa wiki huhakikisha nimekunywa glesi tatu za sharubati hai kukata kiu. Ni kinywaji kinachokabiliana na maradhi ya homa na kifua,” akasema mteja tuliyempata wakati wa mahojiano.

Ukosefu wa malighafi anayotumia kutengeneza sharutabatihai wakati mwingine huwa changamoto. Anasema kuna misimu baadhi ya mimea huadimika, na anayopata ni ghali.

Utengenezaji wa juisi itokanayo na mazao ya shamba unapigiwa upatu kama njia mojawapo wanayofaa kukumbatia wakulima, ili kuyaongeza thamani. Hilo hasa linatiliwa mkazo endapo bei ya mazao kama vile matunda, itakuwa duni ikiwa ni pamoja na kuepuka kero la mawakala au madalali.

Baadhi ya wakulima na hata katika mengi ya masoko, utapata matunda yaliyooza na kutupwa kwa sababu ya kukosa wanunuzi. Wakulima na wafanyabiashara wa matunda wanahimizwa kukumbatia mfumo wa kuongeza mazao ya aina hiyo thamani, kwa kutengeneza juisi.