• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Mahakama yaambiwa Jowie ndiye alikuwa wa mwisho kuonekana na marehemu Monica Kimani

Mahakama yaambiwa Jowie ndiye alikuwa wa mwisho kuonekana na marehemu Monica Kimani

MPENZIWE aliyekuwa mtangazaji katika kituo kimoja cha televisheni, Jacque Maribe, Bw Joseph Kuria Irungu ‘Jowie’ alitambuliwa Jumanne kuwa mtu wa mwisho aliyekuwa na mfanyabiashara Monicah Kimani usiku aliouawa.

Jowie alitambuliwa na Bw Lee Owen Omondi Madala mbele ya Jaji James Wakiaga anayesikiza kesi ya mauaji ya Monicah mnamo Septemba 19 / 20 2018.

Madala alieleza mahakama usiku wa Septemba 19 alienda nyumbani kwa Monicah mwendo wa saa tatu na robo na kumpata Jowie akiwa na mwanamume mwingine aliyemtambua kwa jina moja Walid.

Alisema Walid alitoka kisha akamfuata na kumuacha Jowie aliyesema “ninaweza kulala katika nyumba ya Monicah kwa vile ni kubwa.”

“Nilitoka kwa nyumba ya Monicah mwendo wa saa tano na dakika arobaini na tano usiku na nikamuacha Jowie ambaye Monicah alinieleza atanifuata baada ya muda kidogo lakini nikamsikia Jowie akisema huenda akalala mle kwa sababu nyumba ni kubwa,” Madala alimweleza Jaji James Wakiaga anayesikiza kesi ya mauaji dhidi ya Jacque na Jowie.

Madala aliyekuwa akifanya kazi Sudan Kusini alikuwa ameenda katika makazi ya Monicah yaliyoko eneo la Kilimani, Nairobi kuchukua hati ya umiliki wa gari alilokuwa akisaidiwa na marehemu kubadili usajili.

Madala alisimulia kuwa alifika nyumbani kwa Monicah aliyemlaki.

“Niliwasili katika makazi ya Monicah na nikaelekezwa kwa nyumba yake na bawabu aliyenifungulia lango la kuingia katika Lemure Gardens alikokuwa anaishi mwendazake,” Madala alisema.

Akaendelea: “Nilipobisha mlango Monicah akiwa na furaha alinilaki kwa bashasha na kunielekeza katika chumba cha mazugumzo nilikowapata wanaume wawili wakijiburudisha kwa vinywaji. Monicah alinitambulisha kwao. Alimtaja wa kwanza kuwa Walid aliyesema ni jirani yake. Wa pili alimtambua kwa jina Jowie.”

Shahidi huyu wa pili alisema Monicah alimtambua Jowie kuwa afisa wa usalama katika ofisi ya Rais na wakati huo huo afisa wa usalama katika kitengo cha maafisa wa polisi wa kimataifa (Interpol).

Bw Madala alifichua kwamba Jowie alikuwa amevalia kanzu nyeupe sawa na ya Waislamu, kofia nyekundu na koti la kijivu.

Shahidi huyo alizitambua nguo hizo alipoonyeshwa na kiongozi wa mashtaka Bi Wangui Gichuhi.

Madala alisema Monicah alikuwa amemweleza atasafiri hadi Dubai Septemba 20, 2018, na keshoye alimpigia simu na hakuchukua.

“Nilimpigia simu Monicah na hakuchukua nikafikiri amesafiri. Lakini baadaye nikapokea ripoti kutoka kwa rafiki yangu kwa jina Wanja kwamba Monicah aliuawa usiku niliokuwa naye,” Madala akasimulia.

Jacque na Jowie wamekanusha walimuua Monicah Septemba 19/20 2018 katika eneo la Kilimani Nairobi.

Awali dereva wa teksi John Oketchi alieleza mahakama ndiye alimchukua Monicah kutoka uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta na kumpeleka katika makazi yake yaliyoko Lemure Gardens Kilimani usiku aliouawa

Kesi inaendelea.

You can share this post!

ATUA SPURS: Mourinho ndiye kocha mpya wa Tottenham

Nani yuko salama na nani anakaribia kuaga mbio za kufika...

adminleo