• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Shule zaendelea kufurahia matokeo bora ya KCPE 2019

Shule zaendelea kufurahia matokeo bora ya KCPE 2019

Na SAMMY WAWERU

SIKU tatu baada ya matokeo ya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane, KCPE 2019 kutangazwa, shule mbalimbali zinaendelea kusheherekea matokeo bora.

Mnamo Jumatatu, Waziri wa Elimu Prof George Magoha alitangaza rasmi matokeo hayo.

Sawa na maeneo mengine nchini, hasa shule zilizopata matokeo ya kuridhisha, shule kadhaa katika kaunti ya Nairobi na Kiambu zimeendelea kusheherekea.

Taifa Leo ilifuatilia kwa karibu Jumatano harakati za walimu, wanafunzi na wazazi wa ACK St Andrews School, wakiwa katika harakati za kueneza habari njema za ushindi.

Shule hiyo ya mmiliki binafsi iliyoko eneo la Zimmerman, Kaunti ya Nairobi, ilikuwa na wanafunzi wawili waliopata zaidi ya alama 400 kwa jumla ya 500, zinazowezekana.

Mwanafunzi bora wa alizoa alama 413, akifuatwa na 406.

“Kwa hakika ni kwa neema za Mungu, bidii yetu kama walimu, wanafunzi na ushirikiano wa wazazi kupata hizo,” akasema mwalimu mmoja. Kulingana na mwalimu huyo, matokeo ya mwaka huu yakilinganishwa na mwaka uliopita, ACK St. Andrews imesajili matokeo bora.

Shule ya Edwijet Education Center ambayo pia ni ya binafsi ilikuwa na watahiniwa wawili waliopata zaidi ya alama 400. “Hii ni mara yetu ya kwanza mtahiniwa bora kupata zaidi ya alama 400,” akasema mwalimu mmoja wa shule hiyo, iliyoko eneo la Ruiru, Kiambu.

Barabara na anga za mitaa kadhaa Nairobi na Kiambu, siku tatu zilizopita, zimehinikiza shangwe, vifijo na nderemo hususan shule zilizofanya vyema.

Hata ingawa mtoto wa Simon Muchangi, mkazi wa Kiambu, hakufikisha alama 400, mzazi huyo amesema ana matumaini mwanawe atapata shule bora ya upili.

Shughuli za kusajili wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza mapema 2020, ziling’oa nanga Jumanne na kwa mujibu wa wizara ya elimu zoezi hilo linatarajiwa kukamilika mnamo Desemba 2.

Akitoa matokeo ya KCPE 2019, Prof Magoha alisema serkali imezitatiti kuhakikisha mfumo wa asilimia 100 wanafunzi kujiunga na shule upili unatekelezwa. Aidha, mfumo huo ulianza mwaka jana, kama mojawapo ya ajenda kuu ya serikali ya Jubilee kuimarisha elimu nchini.

Waziri alisema Rais Kenyatta ameamuru zoezi la uteuzi wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza liwe la uhuru, usawa na uwazi.

Jumla ya watahiniwa 1,088,986 walisajiliwa kufanya kufanya KCPE 2019.

You can share this post!

Nani yuko salama na nani anakaribia kuaga mbio za kufika...

Mwanahabari apatikana amefariki chumbani mwa inspekta...

adminleo