Habari Mseto

Niliipata maiti ya Monica kwa bafu, shahidi asimulia mahakamani

November 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

KAKA yake mfanyabiashara Monica Kimani aliyeuawa baada ya kurejea nchini kutoka Sudan Kusini Monica Kimani jana aliambia mahakama kuu walikuta maiti yake ndani ya bafu baada ya kuvunja mlango wa nyumba yake eneo la Kilimani, Nairobi.

“Baada ya Monica kutojibu simu tulizompigia ilibidi niende katika makazi yake kujua kilichojiri kwa vile haikuwa kawaida yake kutojibu simu,” George Kimani alimweleza Jaji James Wakiaga anayesikiza kesi ya mauaji dhidi ya mwanahabari Jacque Maribe na mpenziwe Joseph Kuria Irungu almaarufu Jowie.

George alisema alifululiza hadi kwa makazi ya dada yake yaliyoko Lemure Gardens na kupata mlango umefungwa.

“Nilibisha lakini sikupata majibu.Ilibidi tuuvunje mlango,” alisema George.

Alisema vifunguo vya mlango huo vilikuwa mle ndani na alipoingia alienda kwa chumba cha kulala na Monica hakuwa mle ndani.

Alisema alienda katika bafu na kupata Monica ameuliwa mle ndani.

“Maiti yake ilikuwa ndani ya bafu. Mimi na walinzi na watu wengine tuliita polisi waliofika na kuiondoa maiti yake na kupeleka chumba cha kuhifadhi maiti,” George alimweleza Jaji James Wakiaga anayesikiza kesi hiyo ya mauaji dhidi ya Maribe na Jowie.

Awali George aliambia mahakama Monica alikuwa amemweleza wameanza urafiki na Jowie mwaka wa 2018.

“Je ulikuwa unamjua Jowie hapo mbeleni,”kiongozi wa mashtaka Bi Wangui Gichuhi alimwuliza George.

“Ndio nilimjua Jowie mwaka wa 2012 tukisoma naye katika chuo cha Polytechnic,” George alimjibu Gichuhi.

Shahidi huyu alimweleza jaji kwamba mwaka huo wa 2018 alikutana na Jowie pamoja na dada yake (Monica).

George alikuwa ameandamana na mpenziwe Beautrice Kavata.

“Tulikuwa tumepanga na dada yangu tutaenda Club40 kuburudika. Dada yangu alisema Jowie atajiunga nasi. Jowie alifika na baadaye tukarudi nyumbani mwendo wa saa saba usiku. Tuliporudi , Beautrice alilala na Monica name na Jowie tukalala kwenye viti katika chumba cha mazugumzo,” alisema George.

George alisema dada yake alikuwa akifanya biashara Sudan kusini na alikuwa akirejea nchini mara kwa mara kuwaona watu wa familia yake pamoja na wazazi.

Mkaguzi katika maabara ya Serikali Joseph Kimani aliyekagua nguo na vifaa vingine alivyopelekewa alipata damu ya Monica katika suruali aliyovaa Jowie usiku aliokuwa nyumbani kwa marehemu.

George aliambia Mahakama shingo ya Monica ilikuwa imekatwa.

Jaji Wakiaga alielezwa na shahidi mwingine Jowie ndiye aliachwa na Monica usiku aliouawa mnamo Septemba 19 2018.

Maribe na Jowie wamekanusha walimuua Monica. Maribe yuko kwa dhamana na Jowie alinyimwa akisemekana ni hatari kwa usalama wa mashahidi.

Kesi inaendelea.