JAMVI: Vinara watatu wa Nasa wataziba pengo la 'Baba'?
WYCLIFFE MUIA na CHARLES WASONGA
NI wazi kuwa kinara wa upinzani Raila Odinga atafanya kazi na serikali kutimiza ajenda ya Jubilee ya maendeleo, lakini mjadala unazidi kuibuka kuhusu ni nani atakayechukua nafasi ya Bw Odinga ya kuikosoa serikali ambayo bado ina miaka minne ya kuhudumu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Mwezi mmoja baada ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kusalimiana nje ya Jumba la Harambee, Wakenya wengi bado hawafahamu maafikiano kati ya wawili hao huku vinara wenza katika muungano wa NASA wakiendelea kumkabili Bw Odinga kwa ‘kuwasaliti’ kisiasa.
Vinara wenza katika NASA Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya), sasa wameanzisha mikakati ya kujipanga upya kisiasa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Wadidisi wanasema kibarua cha watatu hao kwa sasa ni kuhusu atakayetoshea katika nafasi ya Bw Odinga kama mkosoaji mkuu wa serikali na kuonekana msemaji wa wafuasi wa upinzani.
“Mwanya ulioachwa na Raila katika upinzani ni mkubwa na yeyote miongoni mwa watatu hao atakayeonekana kujaza nafasi hiyo atakuwa katika nafasi nzuri ya kupambana na (Naibu Rais) William Ruto 2022,” anasema mhadhiri wa masuala ya kisiasa Prof Edward Kisiang’ani.
Fursa kwa Kalonzo
Kulingana na Prof Kisiang’ani, Bw Musyoka ana nafasi nzuri ya kujijenga kisiasa na kukubalika katika maeneo mengi nchini kutokana na siasa zake za kidiplomasia.
“Japo Rais Kenyatta hatamuunga mkono Kalonzo 2022, jamii ya Wagikuyu wanamuamini zaidi kuliko Ruto, lakini itategemea jinsi atakavyojipanga kisiasa kuelekea katika uchaguzi ujao,” anaongeza Prof Kisiang’ani.
Kwa upande mwingine wadadisi wanahisi kuwa Mudavadi na Wetangula wana nafasi nzuri katika kura za 2022 kutokana na idadi kubwa ya kura kutoka magharibi.
Wawili hao tayari wameanzisha mchakato wa kuunganisha vyama vyao vya ANC na Ford Kenya ili waseme kwa sauti moja kisiasa.
Wachanganuzi wanasema kuwa watatu hao wanapaswa kutekeleza kikamilifu wajibu wa kuikosoa serikali ya Jubilee kwa uketo kama Bw Odinga alivyokuwa akifanya kabla ya kubuni ushirikiano na Rais Kenyatta.
Njia ya pekee
“Badala ya watatu hawa kutumia muda wao mwingi kushambulia Raila, wanafaa kujipanga kujaza pengo aliloacha la kuwa mkosoaji mkuu wa serikali. Hii ndiyo njia ya kipekee itakayowafanya kuvutia uungwaji mkono kutoka kwa wananchi,” anasema Bw Vincent Kimosop.
Mchanganuzi huyo anasema inavunja moyo kwamba Bw Musyoka, Mudavadi na Wetangula hawajasema lolote kufuatia hatua ya Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kushambulia Idara ya Mahakama kuhusiana na sakata ya mwanaharakati Dkt Miguna Miguna.
Naye mchanganuzi mwingine Suba Churchil anahofia kuwa huenda taifa likatumbukia katika utawala wa kidikteta endapo hakutakuwa na upinzani thabiti dhidi ya Jubilee.
“Baada ya Raila kuungana na Uhuru, wanasiasa wa upinzani waliosalia ni butu…. hawana ujasiri wa kuikosoa serikali. Kwa kuwa mashirika ya kijamii na vyombo vya habari vimelemazwa na utawala wa sasa kwa kiasi fulani, nahofia kuwa taifa utawala mbaya utakita nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022,” anasema.
Sawa na Kimosop, anawakosoa Musyoka, Mudavadi na Wetang’ula kwa kukumbilia makabila yao “wakati huu ambapo Serikali ya Jubilee inapaswa kukosolewa katika ngazi ya kitaifa”.
Si wageni
“Hawa sio viongozi wageni katika siasa za nchini, kwamba wawili kati yao wamewahi kuwa makamu wa rais. Wanafaa kucheza siasa za kitaifa,” anasema Suba ambaye ni Mshirikishi wa Kitaifa wa Muungano wa Mashirika ya Kijamii.
Ili kuunda chama chenye sura ya kitaifa, Bw Musyoka amepanga kuzuru bara ya Ulaya Juni mwaka huu ili kujifahamisha mengi kutoka kwa vyama komavu vya kisiasa kanda hiyo.
Mwenyekiti wa Wiper Prof Kivutha Kibwana anasema baada ya Wiper kubadilisha jina kuwa One Kenya Movement (OKM), viongozi wa chama hicho wataanzisha kampeni za kitaifa ili kupata uungwaji Kenya nzima.
“Kalonzo anapanga kufanya kikao na Mama Ngina, Seneta Gidion Moi, marais wastaafu Daniel Moi na Mwai Kibaki ili kupata baraka zao hata kama si uungwaji wa kisiasa,”anasema Prof Kibwana.
Nao Seneta Wetangula na Bw Mudavadi wanadaiwa kuanza kumnyemelea Bw Ruto ili mmoja wao awe mgombea mwenza wake 2022.