LEO KUFA KUPONA: Vijana wa Emery wanaalika Southampton
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
SIKU chache baada ya Tottenham Hotspur kufurusha Mauricio Pochettino, macho sasa yako kwa kocha wa Arsenal, Unai Emery, ambaye anahitaji matokeo mazuri haraka upesi, la sivyo akutwe na masaibu sawa na hayo.
Vijana wa Emery wanaalika Southampton uwanjani Emirates leo Jumamosi, huku wadhifa wa Mhispania huyo ukimulikwa zaidi baada ya Arsenal kushinda mechi mbili pekee kati ya 10 zilizopita kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
“Ilikuwa mshangao kwangu,” alisema Emery kuhusu Pochettino kupigwa kalamu. “Nadhani Tottenham ilikuwa inafanya kazi nzuri na Pochettino.
“Pengine, hawakupata matokeo mazuri katika mechi kadhaa zilizopita, lakini kwa jumla nadhani walikuwa wamefanya vizuri chini ya ukufunzi wa Pochettino kwa miaka kadha sasa.”
Emery hajaridhisha mashabiki na wengi wao wanaendelea kukosa amani timu yao inapozoa matokeo duni pamoja na kushindwa kusakata soka ya kupendeza.
Wachanganuzi wengi wa soka walibashiri kuwa kukosekana kwa beki wa kati ndiko kutasababishia Emery matatizo msimu huu wake wa pili, lakini sasa ni wazi kwamba shida kubwa ni katika safu ya ushambuliaji.
Idara hiyo ya mbele ambayo inaongozwa na washambulizi nyota Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette, wakisaidiwa na mchezaji ghali wa Arsenal Nicolas Pepe, mpakuaji shupavu Mesut Ozil, na kiungo Dani Ceballos aliyeajiriwa kwa mkopo kutoka Real Madrid, ilitarajiwa kuwa tegemeo zaidi.
Hata hivyo, watano hao wamefanikiwa kuona lango mara tano pekee katika mechi sita zilizopita za EPL, na kushuhudia Arsenal ikitupwa alama tisa nje ya mduara wa klabu nne-bora.
Aubameyang ameonyesha ukatili wake mbele ya goli kwa kufunga mabao manane licha ya kupata usaidizi mchache. Lacazette na beki wa kati David Luiz ni wachezaji wengine wa Arsenal waliofanikiwa kufunga zaidi ya bao moja ligini msimu huu.
Lacazette hajaona lango katika mechi sita tangu arejee baada ya kupona kifundo, lakini ubutu wa Pepe ndio unapatia Arsenal wasiwasi zaidi.
Raia huyo wa Ivory Coast ametiwa benchi katika mechi mbili zilizopita baada ya kupachika bao moja pekee ligini kwa njia ya penalti.
Ozil uwanjani
Ishara kuwa Emery anatatizika kupata suluhisho zilidhihirika wazi pale alijumuisha Ozil, dhidi ya Wolves; mechi iliyotamatika 1-1 na kupoteza 2-0 dhidi ya Leicester, baada ya kumuacha Mjerumani huyo nje kwa muda mrefu tangu achukue usukani.
Arsenal inaingia mchuano huu na rekodi nzuri. Haijawahi kushindwa na Southampton jijini London katika mechi ya ligi tangu mwaka 1987. Mara ya mwisho Southampton ilizuru uwanjani Emirates, Arsenal ilichabanga wapinzani hawa 2-0 kupitia mabao ya Lacazette na Henrikh Mkhitaryan, ambaye sasa ni mali ya AS Roma.
Ziara ya Southampton, ambayo inashikilia nafasi ya pili kutoka mkiani na haina ushindi katika mechi sita mfululizo ligini, inatarajiwa kupatia Arsenal fursa nzuri ya kufufua kampeni yake. Hata hivyo, matokeo mengine yoyote isipokuwa ushindi, yataweka Emery pabaya zaidi.
“Nimejaa matumaini. Najua tunahitaji mchezo mzuri kutoka kwa kila mchezaji na pia timu nzima,” aliongeza Emery. “Tunahitaji kucheza vyema na kudhibiti mechi dakika zote 90.”
Ceballos anatarajiwa kukosa mechi hii kutokana na jeraha la paja. Hata hivyo, Arsenal inatarajiwa kumkaribisha Granit Xhaka katika mechi hii ambayo Pepe, Aubameyang na Lacazette watategemewa katika utafutaji wa mabao.
Southampton ina wachezaji wakali kama Ryan Bertrand, Danny Ings, Nathan Redmond na James Ward-Prowse.