Makala

UMBEA: Usihangaike bure; furaha yako unayo kiganjani mwako

November 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SIZARINA HAMISI

WANASEMA furaha hutoka moyoni kwa mtu.

Hailetwi sababu ya pesa, hali fulani ya maisha ama watu fulani katika maisha.

Wapo wengine wanaosema kwamba furaha ni uamuzi binafsi wa mtu.

Hata hivyo, hii furaha imekuwa ikitafutwa na wengi bila mafanikio.

Kwamba wengi hudhani wanaweza kupata furaha wanapofikia ama kutimiza hali fulani, kupata vitu fulani, kuwa na uhusiano na watu fulani ama kuwa katika maisha fulani.

Ukweli na hali halisi ni kwamba kulingana na changamoto za mazingira, kiuchumi na kijamii, wapo wale ambao wamejikuta wakikosa furaha.

Ukishatambua kwamba furaha inatoka moyoni kuna mambo kadha ambayo inabidi uwe nayo sambamba ili kupata mzizimo mzuri wa moyoni na hatimaye furaha:

Samehe mara kwa mara

Wahenga walisema kuishi na watu kazi. Hivyo ni muhimu kuelewa jinsi ya kuishi nao, uelewe kwamba hakuna mtimilifu na kila siku yupo ambaye atakukosea ama kukukwaza. Unaweza ukajikuta unakosa furaha kila siku sababu ya kubeba uchungu na maumivu yaliyotokana na watu waliokukosea.

Ikiwa unataka kuwa na furaha ni muhimu kumsamehe aliyekukosea hata kama hajaomba msamaha.

Kumsamehe aliyekukosea kuna manufaa kwako zaidi kuliko kwa yule aliyekukosea. Mara nyingi aliyekosea huendelea na maisha yake ya kawaida huku aliyekosewa akizidi kuumia.

Amua kila siku kwamba ni siku yako ya furaha

Mafanikio siyo ufunguo wa furaha. Furaha ni ufunguo wa mafanikio. Kama unapenda unachokifanya, utafanikiwa. Mojawapo ya siri ya kufanikiwa na kuwa na furaha katika kile unachokifanya, ni kwa kupenda kile unachokifanya.

Iwapo unafanya shughuli ama kazi ambayo ni ya kusukuma siku ziende, na kila siku huna amani moyoni kwako, chukua hatua ya kujikwamua hapo ulipo.

Kuwa na shukrani

Mara nyingi tunatazama mambo mengi kiasi cha kushindwa kuwa na shukrani kwa yale tuliyonayo. Ni rahisi kuona kuwa mambo kama vile afya, marafiki, usalama, na hata malazi ni mambo madogo ambayo hatupaswi kushukuru kwa ajili yake.

Kwa hakika wapo watu wanaotafuta mambo hayo lakini hawayapati. Hivyo ili kupata furaha ni muhimu kutambua na kushukuru kwa yale machache uliyo nayo.

Saidia wengine

Kumsaidia mtu mwingine siyo kumpa pesa au mali bali pia kumpatia ushauri au kumtia moyo kunaweza kuwa na maana kubwa kwa mtu huyo.

Unapomsaidia mtu mwingine unajisikia kuwa na thamani na furaha kwani umeweza kufanya kitu chenye manufaa kwenye maisha ya mtu mwingine.

Shirikisha wengine

Inawezekana jambo linalokukosesha furaha kuna mtu mwingine anafahamu utatuzi wake. Hivyo kwa njia ya kumshirikisha mwingine utapata ushauri au hata utatuzi wa tatizo lako.

Jambo la kuzingatia ni kumshirikisha mtu sahihi ambaye atakupa usaidizi muafaka.

Usitafute ukamilifu

Hakuna mtu mtimilifu, kila mmoja ana kasoro zake. Wote tuna udhaifu na mapungufu ya aina mbalimbali. Badala ya kutafakari udhaifu wako na kuruhusu ukose furaha, jikubali kwamba una mapungufu na uchukue hatua ya kujiboresha.

Muhimu ni wale watu unaoishi nao kila siku, iwapo unajikuta katikati ya watu wanaokulaumu, kukudharau au kukubeza kila wakati, hapo sio mahali sahihi kuwepo.

Iwapo ni muhimu kwako kuwa karibu na watu, hakikisha unakuwa na watu wanaokutia moyo na kukuthamini.

Furaha yako unayo kiganjani kwako.

 

[email protected]