DINI: Ufalme wa mbinguni ni kama karamu ya harusi, unahitaji vazi la kipekee kuingia
NA PADRE FAUSTIN KAMUGISHA
Kila shughuli ina vazi lake. Kuna vazi la kuogelea. Kuna vazi la michezo. Kuna vazi la sikukuu. Kuna vazi la chama cha siasa. Kuna mavazi ya wachungaji wakati wa ibada.
Padre alimuuliza bwana mmoja, “Mke wako alikuwa anakohoa sana leo kanisani.” Bwana huyo akamjibu, “Ni kawaida yake anaponunua vazi la Krismasi.”
Biblia inazungumzia kuhusu vazi la harusi. “Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle ndani mtu mmoja asiyevaa vazi la harusi. Akamuambia, “Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la harusi?” (Mt 22: 11-12).
Vazi hili linawakilisha maisha ya mtu mwokovu yaliyojaa matendo mema. Wakristo wanaonywa dhidi ya ukinaifu; kuishiwa hamu ya kutenda mema.
Hatuwezi kuendelea kuvaa “surupwenye” ya ukatili, chuki, husuda, wizi, ulevi, ubinafsi, mitara, ushirikina na ngoma mbaya, huku tukijidai kuwa wasafi wa moyo.Wakati wa ubatizo Mkristo huwa anavishwa vazi la harusi. Vazi hilo linawakilisha neema ya Mungu. Linawakilisha kuzaliwa upya.
Lazima kulitunza lisichafuke. Kuna kijana aliyetaka kuoa. Akamuendea padre kuomba ushauri. Padre alimtaka ampe vidokezo vya sifa za msichana huyo.
Kijana alisema, “Msichana ni mzuri wa sura”. Padre alichukua karatasi na kuandika chini “0” sifuri. Kijana akasema, “Msichana ni mchapakazi”.
Padre aliandika tena chini “0”. Kijana akaongeza, “Anaimba vizuri”. Padre aliandika chini “0” nyingine.Kijana aliendelea, “Binti ameshinda mtihani wa kuingia Chuo Kikuu”. Padre akaandika tena chini “0”. Kijana akafika tamati kwa kusema, “Msichana ni mkatoliki mzuri sana”.
Hapo Padre akaandika mbele ya sufuri zote, nambari moja ikawa elfu. Funzo hapa ni kwamba, sufuri ziko na maana. Bwana wetu Yesu Kristo anatualika kuingia katika ufalme wa mbinguni akitumia mifano, kama ilivyo desturi yake ya kufundisha.
Kupitia mifano hiyo anawaita watu katika karamu ya ufalme, lakini anataka pia uamuzi wao uwe chaguo la kina: kupata ufalme ni lazima kutoa vyote.
Maneno hayatoshi, unatakiwa matendo. Mifano ni kama kioo kwa binadamu. Je, unapokea neno ukiwa kama udongo mkavu au kama udongo mzuri? Umetumiaje talanta ulizopokea? Yesu anakuhitaji kuvaa vazi linalostahili katika ufalme wake ili kuingia humo.
Lazima uwe mwanafunzi wa Yesu, tayari kuyaacha ya hapa duniani ili kuuona ufalme wa mbinguni. Kwao wanaobaki nje yote yanabaki kitendawili. (Katekisimu ya Kanisa Katoliki Na 546).
Mungu Baba anatualika pazuri pake tangu mwanzo wa dunia. Aliwaalika Adamu na Eva wakae katika bustani ya heri na furaha. Anatualika tena kwa njia ya mwana wake wa pekee Yesu Kristo. Tumfuate yeye kwani ndiye njia ya kwenda mbinguni.
Tupokee mwaliko wake kwa moyo wote. Kupokea mwaliko wa Mungu si suala la kusema “ndiyo” halafu unasahau bali unaendelea kuitikia. Ndiyo si mwisho wa mambo bali mwanzo wa mambo.
Kusema “ndiyo” kwa Mungu ni kama kumaliza shule. Kumaliza shule si mwisho wa elimu. Elimu haina mwisho. Tusome Neno la Mungu na tulifanyie kazi katika maisha yetu.
Myahudi mwenye umri mkubwa akamwendea Rabbii na kumuambia, “Nimeipitia Biblia yote mara tano katika maisha yangu yote.”
Rabbi alimtazama na kusema, “Jambo muhimu si mara ngapi umepitia Biblia bali ni maneno ya Biblia kukupitia.”
Tunapoitikia mwaliko tunahitaji kuridhika. Tumuige mtume Paulo aliyesema, “Nimejizoesha kuridhika katika kila hali.
Naweza kuikabili kila hali kwani Kristo hunipa nguvu.” (Wafilipi 4: 11-12). Kuridhika kwa Paulo ni kwa sababu aliweka mizizi yake katika Yesu Kristo. Lakini kuna kutoridhika chanya: hatupaswi kuridhika na umaskini na ujinga.