• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
Demu aliyekataa kupika afurushwa

Demu aliyekataa kupika afurushwa

Na TOBBIE WEKESA

KITALE MJINI

Kizaazaa kilizuka katika ploti moja mtaani humu baada polo kumfurusha kidosho mpenzi wake alipokataa kuingia jikoni kupika

Inasemekana polo aliudhika sana baada kipusa kumwambia hangeingia jikoni kupika.

Kulingana na mdokezi, mrembo alikuwa ameenda kumtembelea polo kwake. Inadaiwa polo alinunua kila kitu ambacho kilihitajika jikoni kwa mapishi.

Duru zinasema mrembo alipowasili, polo alimuandalia kinywaji cha soda na baada ya muda kipusa akasema alikuwa akihisi njaa.

“Beib nina njaa sana. Nilipotoka kwangu sikuwa nimekula chochote,” mrembo alimueleza polo. Polo aliingia jikoni na kuhakikisha kila kitu kilikuwa sawa. “Nimetoka kufanya shoping sasa hivi. Ingia jikoni upike,” polo alimueleza mrembo.

Duru zinasema mrembo alibaki ameketi kochini huku akimuangalia polo kwa mshangao. “Beib unataka niingie jikoni kufanya nini?” kipusa alimuuliza polo.

Inadaiwa polo alinyamaza tu. “Mimi sitaingia jikoni. Nenda ukanunue chakula kilichopikwa tayari supamaketi,” kipusa alimueleza polo.

Kimzaha tu, polo alimuuliza kidosho angependa kununuliwa chakula kipi. “Nunua kuku nusu, soda, soseji na chipsi,” kipusa alimueleza jamaa. Inadaiwa jamaa alimrai kidosho agharamie chakula hicho. “Mimi sina hela. Siwezi kuja kwako na niingie jikoni nipike. Ukitaka acha chakula chako kikae,” kipusa aliapa

Kulingana na mdokezi, hasira zilianza kumpanda polo. “Ni mimi unaambia hivyo ama kuna mtu mwingine. Toka kwa nyumba yangu haraka,” alimfokea kidosho.

Kidosho alibaki ametulia tu kochini huku akifikiria jamaa alikuwa akifanya mzaha. “Hata sijaona faida ya kuja kwangu,” polo alimfokea kipusa. Inadaiwa polo alimkaribia kidosho na kumuinua kutoka kochini na mwanadada akachomoka bila kuangalia nyuma.

“Nenda kabisa. Usiwahi kurudi tena kwangu,” polo alimfokea kidosho.

 

You can share this post!

DINI: Ufalme wa mbinguni ni kama karamu ya harusi,...

JAMVI: Je, ni njama Mlima Kenya kuhujumiwa kiuchumi?

adminleo