• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
JAMVI: Je, ni njama Mlima Kenya kuhujumiwa kiuchumi?

JAMVI: Je, ni njama Mlima Kenya kuhujumiwa kiuchumi?

Na WANDERI KAMAU

JE, huenda hali ngumu ya kiuchumi inayolikabili eneo la Mlima Kenya ni njama ya serikali ya Jubilee kuwafilisisha wananchi kimakusudi?

Hilo ni mojawapo ya maswali makuu ambayo yameibuka miongoni mwa wananchi, viongozi na wachanganuzi wa kisiasa kufuatia mkutano wa viongozi mbalimbali wa kisiasa wa eneo hilo ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta katika eneo la Sagana, Kaunti ya Nyeri wiki iliyopita.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wanasema kuwa Rais Kenyatta aliyafumbia macho kimakusudi malalamishi ya wenyeji kuhusu kudorora kwa hali ya kilimo, licha ya kufahamu hali ilivyo.

Licha ya wengi wao kutotaka kuonekana hadharani wakitoa kauli zao, baadhi wanaungama kwamba huenda kimya cha Rais kinaashiria hali ya kutojali kwa serikali kuhusu changamoto hizo.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria anasema kuwa mkutano huo ulikosa maana yoyote kwani hakuna kipya kilichojadiliwa.

“Tulikuwa hapa mnamo 2016. Sijasikia lolote lipya ambalo lilielezwa. Hivyo, sioni maana yoyote ya kikao hicho,” akasema Bw Kuria.

Mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua anaunga mkono kauli hiyo, akisema kuwa jamii ya Agikuyu ndiyo inayoathirika zaidi na ugumu wa kiuchumi uliopo nchini.

Watu mbalimbali waliohudhuria mkutano huo waliwakosoa vikali wale walioteuliwa kuhutubu, wakisema kuwa walianza kumsifu Rais Kenyatta, badala ya kumweleza hali halisi ilivyo.

Mmoja wao ni Bw Zac Kinuthia, aliyeteuliwa kuzungumza kwa niaba ya vijana. Duru zinaeleza alizomewa vibaya alipoanza kueleza jinsi serikali ya Rais Kenyatta ilivyojitolea kuwasaidia vijana.

“Kilicho dhahiri ni kwamba wazungumzaji walioteuliwa walimpotosha Rais Kenyatta kuhusu hali halisi ilivyo. Tunashangaa ikiwa hili lilifanyika kimakusudi ama ni jambo lililopangwa,” akasema Bw Gachagua.

Wachanganuzi wanasema kuwa Rais Kenyatta anafahamu hali ya kiuchumi ilivyo ikizingatiwa kuwa biashara nyingi za familia ya Kenyatta zinajikita katika masuala ya kilimo.

Familia ya Mzee Jomo Kenyatta inamiliki Kampuni ya Brookeside, ambayo huwanunulia wakulima maziwa.

Familia hiyo vilevile inamiliki Benki ya CBA (Commercial Bank of Africa) ambayo majuzi iliungana na benki ya NIC na kuwa NCBA.

Wakulima wengi wanalalamika kwamba bei ya maziwa imeshuka kutoka wastani wa Sh38 mnamo 2017 hadi Sh17 mwaka huu.

Wafanyabiashara wanaohusika katika biashara ya vipuli vya magari pia wamekuwa wakilalamikia kodi za juu, kunaswa kwa shehena za mizigo yao na kuhangaishwa na asasi mbalimbali za serikali, hali ambayo imewafanya wengi wao kufunga biashara zao, hasa katika eneo la Nyamakima, jijini Nairobi.

Mnamo Mei, Rais Kenyatta alikiagiza Kitengo cha Kukagua Shehena katika eneo la Embakasi kuachilia shehena za wafanyabiashara hao ambazo zilikuwa zimezuiliwa katika eneo hilo.

Rais alifika katika eneo hilo baada ya vilio na malalamishi kutoka kwa wafanyabiashara hao.

“Nawaagiza wasimamizi wakuu wa idara hii kuachilia shehena hizo kwa muda wa majuma matatu ili kuhakikisha wafanyabiashara wetu hawateseki tena,” akasema Rais Kenyatta.

Kando na hayo, sekta ya miraa pia imeathiriwa vikali, huku ikiibuka kwamba bajeti ya kuimarisha zao hilo imepunguzwa kutoka Sh1 bilioni hadi Sh400 milioni kama Rais alivyoahidi mwaka jana.Wachanganuzi wanasema kuwa ni kawaida kwa watawala kuwafilisisha kimakusudi raia, ili “kukuza zaidi uzalendo wao.”

“Hii ni mbinu ya kisiasa ambayo imekuwa ikitumika kwa muda mrefu na wanasiasa, hasa wanapopania kuzima maasi yoyote miongoni mwa raia. Hili huhakikisha kuwa wanawaona kama ‘mwokozi wao’ pale wanapotangaza mikakati ya kufufua uchumi,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Prof Ngugi Njoroge, anayesema kuwa mbinu iyo hiyo ndiyo aliyotumia Rais Mstaafu Daniel Moi dhidi ya jamii ya Agikuyu alipohudumu kama rais kwa miaka 24.

“Kwa kuogopa uwezo mkubwa wa kiuchumi wa jamii ya Agikuyu, Bw Moi alihakikisha kwamba amesambaratisha sekta muhimu kama kilimo ili kuizima jamii hiyo kiuchumi. Vile vile, aliihujumu kisiasa kwa kuhakikisha kuwa hakuna viongozi walioteuliwa katika nyadhifa kuu serikalini,” asema Prof Njoroge.

Rais Kenyatta amekuwa akilaumiwa pakubwa kwa kutowachukulia hatua mawaziri Mwangi Kiunjuri (Kilimo) na Peter Munya (Biashara na Viwanda) kwa kutowajibikia vizuri utendakazi wao.

Wenyeji wengi wa Mlima Kenya wanasema kuwa ni kinaya kwamba mawaziri hao wanasimamia sekta muhimu ambazo ndizo nguzo kuu za kiuchumi kwa eneo hilo.

“Ikiwa Rais Kenyatta angekuwa anachukulia malalamishi ya wenyeji wa Mlima Kenya kwa uzito, angewafuta kazi mara moja mawaziri Kiunjuri na Munya, kwani wanasimamia sekta zinazohimili uchumi wa eneo hilo,” akasema mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri.

Rais Kenyatta amemwonya Bw Kiunjuri hadharani mara kadhaa, hasa baada ya kuibuka kwa sakata ya mahindi ambapo wakulima ghushi wanadaiwa kulipwa zaidi ya Sh1.8 bilioni kwa kuwasilisha mahindi yao kwa Halmashauri ya Kitaifa ya Ununuzi wa Nafaka (NCPB).

Hata hivyo, baadhi wanafasiri kwamba maonyo hayo hayana maana yoyote, kwani mawaziri hao wanaendelea kuhudumu bila kuogopa.

You can share this post!

Demu aliyekataa kupika afurushwa

JAMVI: Wabunge wa Mlima Kenya wanavyohadaa watu kuhusu BBI

adminleo