MakalaSiasa

JAMVI: Wazika tofauti zao kisiasa, masaibu ya Mutua yaanza nyota yake ikiangamizwa!

April 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na WYCLIFFE MUIA

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka na Gavana wa Kitui Charity Ngilu wamezika tofauti zao za kisiasa katika kaburi ambalo linatishia kumeza kisiasa mahasidi wa Bw Musyoka akiwemo Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua. 

Kwa miaka mingi, siasa za Ukambani zimegubikwa na uhasama wa kisiasa kati ya Bi Ngilu na Bw Musyoka lakini sasa viongozi hao wawili wameamua kuunganisha vyama vyao vya kisiasa na kuweka kura za Wakamba katika kapu moja.

Wadadisi wasema huenda umoja huu ukaua ndoto ya kisiasa ya Dkt Mutua iwapo hatajiunga na viongozi hao wawili wenye ushawishi mkubwa eneo la Ukambani.

Katika mkutano wa kisiasa ulioandaliwa Jumatatu eneo la Matungulu, Kangundo, Bi Ngilu ambaye ni mwenyekiti wa chama cha Narc, aliwaonya wanasiasa wanaolenga kugawanya kura za Ukambani kuwa wataambulia patupu.

“Nilikuwa kigogo pekee kutoka Ukambani aliyepinga mtoto wetu (Kalonzo) katika chaguzi za nyuma lakini sasa namuunga mkono. Sharti tuungane pamoja ili kulinda kura zote za Wakamba, tumpe Kalonzo nguvu za kushawishi jamii nyingine kuelekea 2022,”alisema Bi Ngilu.

Bila kumtaja Gavana Mutua moja kwa moja, Bi Ngilu aliahidi kuua mirengo mingine inayochipuka Ukambani na kumshauri Bw Musyoka atafute kura maeneo mengine bila kuyumbishwa na ‘sauti ndogo’ ya waasi Ukambani.

“Niachie eneo la Ukambani nitakuletea kura zote zaidi ya milioni nne…nendeni ukasake wanasiasa wengine uko nje wakujazie kura za urais,”Bi Ngilu alimshauri Bw Musyoka.

Punde baada ya mkutano huo wa Matungulu, Gavana Mutua alipuuzilia mbali umoja wa viongozi hao akisema hautadumu.

Aliutaja kama mkutano wa chama cha Wiper na wala si wa viongozi wa Ukambani na kuwa, ulilenga tu kufufua nyota ya kisiasa ya Bw Musyoka.

 

Mkutano wa Mutua

Kiongozi huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap aliapa kuandaa mkutano mkubwa wa kisiasa unaowahusisha viongozi ‘halisi’ wa Ukambani, wakiwemo wakuu wa makanisa na wafanyabiashara wa eneo hilo.

Wengine ambao wanaegemea upande wa Dkt Mutua ni pamoja na wabunge Victor Munyaka (Machakos Mjini), Rachael Nyamai (Kitui Kusini) na Nimrod Mbai (Kitui Mashariki) wote ambao walisusia mkutano wa Matungulu.

Wabunge hao waliochaguliwa kupitia chama cha Jubilee hata hivyo wametofautiana na mpango wa Dkt Mutua kutaka kuwania urais 2022 kwa sababu wao wanaunga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto.

Bi Ngilu na mwenzake wa Makueni Prof Kivutha Kibwana walipuuzilia mbali uasi wa wabunge hao wakisema, hauna athari zozote za kisiasa kwa umoja wa viongozi wa Ukambani.

Prof Kibwana alilinganisha uasi wa Dkt Mutua na ‘beberu wadogo wanaoiga tabia ya beberu wakomavu kutunga mbuzi mimba.’

“Katika boma kuna beberu komavu anayezalisha mbuzi wale waliokomaa katika zizi. Lakini pia unapata kuna beberu wadogo wanaojaribu kupanda mama zao ili kuigiza wenzao wakubwa,”alisema Prof Kibwana huku umati ukiangua kicheko.

 

Mutua ni beberu mdogo

Gavana huyo alisema kwa kawaida, beberu wakubwa hawajalishwi na tabia za beberu wadogo hivyo kina Mutua na wenzake hawapaswi kukemewa kwa kutohudhuria mkutano huo.

Japo Dkt Mutua alisema hakupata mwaliko, aliyekuwa mbunge wa Afrika Mashariki Peter Mathuki aliambia Taifa Jumapili kuwa, Gavana Mutua alipigiwa simu na Bw Musyoka akimualika.

“Hisia za Dkt Mutua baada ya mkutano huo ni ushahidi tosha kuwa alikosa nafasi nzuri ya kurudi nyumbani,”alisema Bw Mathuki.
Wakili Duncan Ojwang’ asema ingemfaa sana Dkt Mutua iwapo angehudhuria mkutano huo ulioandaliwa na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama.

“Ni vyema kuvuka mto na watu wengi ili kuepuka kutafunwa na mamba. Ukivuka peke yako utanaswa virahisi sana na mamba,” Dkt Ojwang’ akitumia mafumbo kueleza hali ya kisiasa ya Dkt Mutua na wenzake kutoka Ukambani.

Dkt Ojwang’ anahisi kuwa, Bw Musyoka amefanikiwa kudhibiti kura za Ukambani kwa kuungana na Bi Ngilu, hivyo Gavana Mutua hatakuwa na ushawishi wowote wa kisiasa ifikiapo 2022.

 

Mutua hajafikia Kalonzo

“Kabila ndio taasisi kubwa ya kisiasa nchini inayoamua nani ataunda serikali katika siasa za Kenya. Dkt Mutua anaweza kuwa na maoni tofauti na viongozi wa Wiper lakini ukweli mchungu ni kuwa, hana uungwaji mkono wa kisiasa eneo hilo kama Kalonzo,”alisema Dkt Ojwang.’

Hata hivyo, wakili Philip Magal anahisi muungano wa Ngilu na Bw Musyoka ungekuwa na nguvu zaidi iwapo wangemshirikisha Gavana Mutua.

“Gavana Mutua amekuwa sura ya ugatuzi tangu 2013 na japo hangeweza kushawishi Wakamba kumpigia kura Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2017, huenda akawa na ushawishi ifikiapo 2022,”asema Bw Magal.

Naye mchanganuzi wa kisiasa Brian Mutie asema ni mapema kusherehekea umoja wa Bi Ngilu na Bw Musyoka.

“Uchaguzi wa 2022 uko mbali sana na chochote kinaweza kutokea. Kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika, kutachipuka mirengo mingi na haijulikanani iwapo umoja wa wawili hao utadumu hadi 2022,” anaonya Bw Mutie.

Gavana Mutua tayari ametangaza kuwania urais 2022 baada ya kumaliza muhula wake wa pili wa ugavana, na azma ya urais ya Bw Musyoka huenda ikaathiri ndoto yake.

Aliyekuwa mbunge wa Mwingi ya Kati, Joe Mutambu alisema viongozi wa chama cha Jubilee eneo la Ukambani wataandaa mkutano wao wa kisiasa hivi karibuni ili kutoa mweleko wao.