BBI: Baadhi ya mawaziri kuteuliwa kutoka miongoni mwa wabunge
Na CHARLES WASONGA
BAADHI ya mawaziri watateuliwa kutoka bunge endapo pendekezo la Jopo la Maridhiano (BBI) litaidhinishwa na asasi husika pamoja na Wakenya.
Katika ripoti iliyowasilishwa rasmi kwa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga katika Ikulu ya Nairobi, jopo hilo linaloongozwa na Seneta Yusuf Haji linasema kuwa wataalamu ambao pia watateuliwa katika baraza la mawaziri watahudumu kama wabunge maalum.
“Mawaziri watateuliwa kutoka miongoni mwa wabunge na wataalamu. Na baada ya uteuzi wao kuidhinishwa na bunge, wataalamu hao pia watahudumu kama wabunge,” muhtasari wa ripoti hiyo ambayo Taifa Leo imepata Jumanne unasema.
Na mawaziri hao watateuliwa na Rais kwa kushauriana na Waziri Mkuu baada ya Rais mwenyewe kubuni nafasi za uwaziri.
Kulingana na jopo hilo la watu 14, uteuzi wa baadhi ya mawaziri miongoni mwa wabunge utatoa mwelekeo wa kisiasa na uwajibikaji kwa bunge miongoni mwa mawaziri.
“Mfumo wa sasa ambapo mawaziri wanateuliwa kutoka nje ya bunge umeleta hali ya mkanganyiko baina ya bunge na serikali kuu. Hamna ukuruba kati ya wabunge na mawaziri na ndiposa Wakenya waliofika mbele yetu kuwasilisha maoni yao walipendekeza baadhi ya mawaziri wateuliwe kutoka bunge,” ripoti hiyo ikasema.
Na wale wabunge ambao watateuliwa kuwa mawaziri wataendelea kupokea mshahara wao kama wabunge kwani hawataongezewa mshahara zaidi, kulingana na BBI.
Pendekezo hili tayari liko kwenye vielelezo vya miswada ya marekebisho ya Katiba ambayo imeandaliwa na wabunge; William Kamket (Tiaty) na Vincent Kimose (Mugirango Magharibi).
Katika miswada hiyo ambayo haijawasilishwa rasmi bungeni ili kujadiliwa, wabunge hao wanapendekeza kufanyiwa mabadiliko kwa kipengee cha 152 (3).
“Uteuzi wa mawaziri miongoni mwa wabunge utawapa wabunge nafasi ya kuwauliza wabunge maswali na kupata ufafanuzi papo hapo. Ilivyo sasa ni kwamba baadhi ya mawaziri wamekuwa wakikwepa kufika mbele ya kamati za bunge wanapohitajika kujibu maswali kwa sababu wanawajibika moja kwa moja kwa afisi ya rais badala ya asasi ya bunge inayowasilisha wananchi,” anasema Bw Kemosi.
Kumekuwa ni mikwaruzano kati ya wabunge na mawaziri tangu 2013 chini ya mfumo wa sasa kwani baadhi ya mawaziri wamekuwa wakikaidi mialiko ya kufika bunge wakidai “kuzongozwa na majukumu ya afisi zetu”
Baadhi ya mawaziri ambao wamekosana na wabunge kwa njia hii ni Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’I na mwenzake wa Uchukuzi James Macharia.
Kulingana na ofisi ya bunge inayosimamia masuala ya bajeti (Parliamentary Budget Office-PBO), pendekezo la kuteua mawaziri kutoka bunge linaweza kuokoa mamilioni ya pesa kila mwaka, endapo idadi ya juu zaidi ya mawaziri itasalia kuwa 22.
Hii ni kwa sababu wabunge ambao watateuliwa kuwa mawaziri hawatapokea mishahara zaidi isipokuwa marupurupu madogo ya kimajukumu.
Kulingana na mwongozo wa mishahara uliotolewa na Tume ya Mishahara (SRC) Julai 1, 2018, waziri hupokea Sh924,000 kama mshahara na marupurupu, kila mwezi. Hii ina maana kuwa serikali hutumia jumla ya Sh243.9 milioni kila mwaka kugharimia mishahara na marupurupu ya mawaziri.
PBO, katika ripoti yake ya Aprili 2019 inasema kuwa endapo mawaziri watateuliwa kutoka miongoni mwa wabunge gharama hiyo itapungua hadi Sh105.6 milioni kila mwaka.